1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Hali ya usalama bado ni ya mashaka mji mkuu wa Haiti

19 Machi 2024

Polisi nchini Haiti inaendelea kukabiliana na magenge ya uhalifu ambayo yamezidi kujiimarisha katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Port-au-Prince ambako watu 10 wameripotiwa kuuawa hapo jana.

https://p.dw.com/p/4dt3n
Haiti Port-au-Prince
Polisi mjini Port-au-Prince Haiti wakilinda doriaPicha: Odelyn Joseph/AP/dpa/picture alliance

Polisi nchini Haiti inaendelea kukabiliana na magenge ya uhalifu ambayo yamezidi kujiimarisha katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Port-au-Prince ambako watu 10 wameripotiwa kuuawa hapo jana katika kitongoji wanakoishi matajiri cha Petion-Ville.

Magenge hayo ya wahalifu yalishambulia pia makazi ya watu, benki na kituo cha mafuta katika eneo hilo. Nchi hiyo ya Carribean imetumbukia katika hali ya sintofahamu kisiasa kufuatia tangazo la hivi majuzi la kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Ariel Henry.

Umoja wa Mataifa, Marekani na Shirika la kikanda Caricom wanaunga mkono kuundwa kwa baraza la mpito la kisiasa. Kufuatia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Haiti uliofanyika jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamaica Kamina Johnson Smith amesema mazungumzo ya uundwaji wa baraza hilo yanaendelea vyema.