1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milio ya risasi yaendelea kurindima Haiti

Sylvia Mwehozi
15 Machi 2024

Milio ya bunduki ilisikika kote kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince hapo jana, na magenge ya wahuni yaliichoma moto nyumba ya afisa wa polisi.

https://p.dw.com/p/4ddAL
Haiti | Port-au-Prince
Haiti bado hali ni tete, milio ya risasi inarindima wakati wanasiasa wakijaribu kuunda baraza la mpitoPicha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Ghasia hizo za jana zimevuruga hali ndogo ya utulivu iliyoripotiwa kwa siku tatu wakati wanasiasa wakiendeleza mazungumzo ya kuunda baraza la mpito la uongozi.

Hali bado ni mbaya katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince

Nje kidogo ya mji mkuu wa Port-au-Prince, majambazi walipora na kisha kuchoma moto nyumba ya mkuu wa jeshi la polisi huko Santo. Polisi mmoja anaripotiwa kupigwa risasi na kujeruhiwa katika eneo la makao makuu ya polisi karibu na uwanja wa ndege. 

Naye kiongozi mmoja wa mtandao wa magenge ya wahalifu nchini humo Jimmy Cherizier maarufu kama "Barbeque" ametoa ujumbe wa vitisho kwa viongozi wa kisiasa watakaojiunga kwenye baraza la mpito la utawala, wakati hali ikizidi kuzorota katika mji mkuu wa taifa hilo.