1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: K.Kaskazini imepeleka makombora na wanajeshi Urusi

Angela Mdungu
14 Oktoba 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Korea Kaskazini imepeleka wanajeshi na makombora ya masafa marefu Urusi yatumike katika vita dhidi ya taifa lake.

https://p.dw.com/p/4ll9D
Zelesky ameituhumu Korea Kaskazini kuipa Urusi makombora ya masafa marefu
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Rais huyo wa Ukraine amezungumzia pia ushirikiano wa karibu kati ya tawala za mataifa hayo mawili ambapo ameeleza kuwa hivi sasa kunashudiwa uhusiano unaozidi kukua kati ya Urusi na utawala wa mataifa kama Korea Kaskazini. Ameeleza kuwa uhusiano huu si tu wa kupeleka silaha bali pia ni wa kupeleka wanajeshi kutoka Korea Kaskazini kwenda kwa vikosi vya Urusi.

Amesisitiza kuwa kutokana na hatua hiyo,ni wazi kuwa katika mazingira kama hayo uhusiano wa Ukraine na washirika wake unapaswa kuendelezwa zaidi.

Licha ya tuhuma  zilizotolewa na Zelensky, bado hakujawa na uthibitisho huru kuwa wanajeshi wa Korea ya Kaskazini wanashirikiana na Urusi katika vita dhidi ya Ukraine. Zelensky hata hivyo anakusudia kuzungumza na washirika wake wa mataifa ya magharibi kuhusu suala hilo.

Zaidi ya watu 30,000 wamehamishwa mpakani kuepuka mapigano Urusi

Kwingineko, kamishna wa haki za binadamu nchini Urusi Tatyana Moskalkova, amearifu kuwa, takriban watu 30,415 wakiwemo watoto 8,000 wamehamishwa kutoka katika maeneo yanayopakana na Ukraine kutokana na mashambulizi.

Akizungumza wakati wa mahojiano na shirika la habari la Argumenty I Fakty Moskalkova amesema watu hao wamepelekwa katika takriban vituo 1,000 vya makazi ya muda kote nchini Urusi.

Itakumbukwa kuwa, wanajeshi wa Ukraine mnamo mwezi Agosti walifanya uvamizi wa kushtukiza katika mkoa wa Kursk ambao ni eneo la Urusi, na kuyateka maeneo kadhaa. Hadi sasa bado inaendelea kuyashikilia baadhi ya maeneo hayo.

Kyiv, ilifanya uvamizi wa ghafla Urusi katika mkoa wa Kursk
Moja ya mashambulizi ya Ukraine katika mkoa wa Kursk, UrusiPicha: IMAGO/SNA

Soma zaidi: Urusi na Ukraine zashambuliana kwa droni na makombora

Katika hatua nyingine, Ukraine imesema Jumatatu kuwa imeiangamiza ndege ya jeshi ya Urusi mwishoni mwa Juma. Kwa mujibu wa shirika la kiitelijensia la Kyiv, ndege hiyo chapa Tu-134 ilishambuliwa usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili katika uwanja wa ndege wa jeshi wa mkoa wa Orenburg nchini Urusi Kilomita 1,000 kutoka katika eneo la mpakani.  Kwa upande wake Urusi haijatoa kauli yoyote kuhusu shambulio hilo.      

Wakati huohuo, mawaziri wa mabo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wamepitisha azimio la kuiwekea vikwazo Iran kutokana na taifa hilo kuipa Urusi makombora ya masafa marefu ili yatumike katika vita dhidi ya Ukraine. Kulingana na wanadiplomasia, vikwazo hivyo vimeyalenga makampuni na watu waliohusika katika programu ya makombora ya masafa marefu ya Iran, na kupeleka silaha hizio na nyingine Urusi.