1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANZIBAR : Wazanzibari leo wapiga kura katika uchaguzi mkuu

30 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CENM

Wapiga kura katika visiwa vya Zanzibar nchini Tanzania wanapiga kura leo katika uchaguzi wenye ushindani mkali wa Rais,wajumbe wa baraza la wawakilishi na madiwani huku kukiwa na ulinzi mkali,vurugu za hapa na pale na madai ya udanganyifu.

Katika mji mkongwe mji wa kale na kitovu cha utamaduni katika visiwa vya Zanzibar wapiga kura waliokuwa wakisubiri kupiga kura katika vituo viwili vya kupigia kura walipambana na kile kinachodaiwa kuwa ni wapiga kura bandia ambao wamesema wameletwa na chama tawala cha CCM.

Katika eneo mashuhuri la ufukweni la Forodhani wapiga kura walivurumisha mawe na kutembeza bakora kwa makundi matatu tafauti ya wapiga kura wanaosema kwamba wameletwa kutoka nje ya eneo hilo.

Baadhi ya wapiga kura hao walithibitisha kwa shirika la habari la AFP kwamba sio waakazi wa Forodhani ambayo ni ngome kuu ya chama cha upinzani cha CUF lakini wamepelekwa hapo kwa nguvu na viongozi wa CCM.

Hali kama hiyo pia imeripotiwa kutokea katika ngome kuu nyengine ya CUF Malindi ambapo wapiga kura wamewashutumu wanawake wanaosema kuwa wametoka nje ya eneo hilo.

Rais Amani Abeid Karume amewaambia waandishi wa habari wakati akipiga kura yake katika eneo la Kiembesamaki kwamba anafikiri uchaguzi huo utakuwa wa amani kinyume na vile watu wanavyofikiria.

Mpinzani mkuu wa Karume Seif Sharrif Hamad wa chama cha CUF ambaye alipoteza chaguzi mbili zilizopita ameapa kufanya maandamano makubwa kama yale ya Ukraine iwapo uchaguzi huu wa leo utafanyiwa udanganyifu.

Uchaguzi huo wa Zanzibar ni mtihani wa sifa ya Tanzania kama kielelezo cha utulivu kwa Afrika.