1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANZIBAR: Majina 700 ya uwongo yagunduliwa kwenye daftari la wapiga kura

21 Septemba 2005
https://p.dw.com/p/CEZB

Jopo la uchaguzi visiwani Zanzibar limearifu kwamba limegundua majina zaidi ya 700 ya uwongo kwenye orodha ya wapiga kura visiwani humo.

Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC imesema majina hayo yaligunduliwa na wataalamu visiwani humo wanaolisaidia jopo hilo katika kuhakiki orodha ya wapiga kura baada ya serikali kufutilia mbali kandarasi na kampuni ya Afrika Kusini iliyokuwa imepewa jukumu la kuhakiki orodha hiyo mnamo mwezi Agosti uliopita.

Kwa mujibu wa kiongozi wa tume ya uchaguzi Zanzibar bwana Masauni Yusuf Masauni kwenye zoezi hilo kumepatikana majina ya watu 700 yaliyo na hitilafu ikiwa ni pamoja na mengine kuandikishwa mara mbili.

Afisa mmoja wa tume hiyo ya Uchaguzi ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari ya AFP kwamba shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP limechukua jukumu la kuhakikisha kwamba orodha ya wapiga kura imepitiwa barabara baada ya kampuni ya Afrika Kusini kunyimwa jukumu hilo.