Wolfsburg yahifadhi kombe la Champions League kwa wanawake
23 Mei 2014Wolfsburg walionyesha mchezo wa hali ya juu katika kipindi cha pili, kwa kutoka nyuma magoli mawili kwa sifuri na kuwashinda wapinzani wao wa Sweden Tyresö FF katika fainali ya Champions League.
Kocha wa Wolfsburg Ralf Kellermann amesema timu yake ilicheza vyema kabisa katika kipindi cha pili, na hivyo anajivunia sana. Wolsfburg ambao hawakupigiwa upatu kabla ya mechi hiyo, dhidi ya timu ambayo inaongozwa na nyota wa Brazil Marta, ilionekana kuwa dhaifu kabla ya kwenda mapumzikoni.
Marta alifungua ukurasa wa magoli katika dakika ya 28, muda mfupi kabla ya mchezaji aliyempa paso Veronica Boquete kuongeza la pili baada ya nusu saa ya mchezo. Mashabiki 8,000n waliokuwa katika uwanja wa Estadio de Restelo wangesamehewa kwa kutarajia kipindi kibovu cha pili.
Wolfsburg kisha waliwabumburusha Tyresö baada ya kipindi cha kwanza wakati Alexandra Popp alipofunga kwa njia ya kichwa katika dakika ya 47. Katika dakika ya 53, Wolfsburg walisawazisha kupitia mshindi wa tuzo ya mchezaji bora mwanamke wa Ujerumani Martina Müller, ambaye pia ni nahodha wa kikosi hicho.
Nyota wa Brazil Marta kisha akadhihirisha ni kwa nini alishinda tuzo ya mchezaji bora mwanamke wa mwaka katika misimu mitano mfululizo, kwa kuwarejesha Wasweden kifua mbele. Verena Faisst, aliingia kamanguvu mpya na kuwasawazishia Wolfsburg katika dakika ya 68, kabla ya nahodha Müller kutikisa wavu na kuwapa wajerumani hao ushindi.
Rais wa shirikisho la soka Ujerumani Wolfgang Niersbach na Rais wa UEFA Michel Platini walikuwa miongoni mwa wageni mashuhuri waliokuwa katika umati wa mashabiki.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef