1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Mzozo wa virusi vya corona utakuwa wa muda mrefu

23 Aprili 2020

Shirika la Afya Duniani WHO limeonya kuwa mzozo wa virusi vya corona hautamalizika hivi karibuni kutokana na mataifa mengi kuwa kwenye hatua za mwanzo za kupambana na virusi hivyo hatari.

https://p.dw.com/p/3bHHQ
Tedros Adhanom Ghebreyesus Direktor WHO
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Ghebreyesus Picha: Getty Images/AFP

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus amesema itakuwa ni kosa kubwa kuharakisha kuondowa haraka vizuizi vya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona kwa sababu hali bado haijatengamaa.

Ghebreyesus ameongeza kusema wakati mataifa mengi yako katika siku za mwanzo za mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19, nchi zilizoathiriwa mapema zinashuhudia wimbi jipya la maambukizi.

Mkuu huyo wa shirika la WHO pia ameendelea kuhimiza umuhimu wa kuwepo mshikamano duniani katika vita dhidi ya virusi vya corona

"Na iwapo kutakuwa na mshikamano wa ulimwengu, na kuichukulia kadhia hii kuwa adui wa wote wa ubinadamu na kujitoa kikamilifu huku tukitambua kwamba kirusi hiki ni kipya na ni hatari - tunaweza kushinda. Bila ya hilo, bila ya umoja wa kitaifa na mshikamano wa kimataifa, tunawaambiene hali mbaya zaidi iko mbele yetu. Kwa pamoja tuzuie janga hili." amesema Ghebreyesus

Tahadhari ya wimbi la pili yatolewa Marekani 

USA | Donald Trump | Coronavirus Briefing
Picha: Reuters/J. Ernst

Onyo la WHO limetolewa wakati wataalamu wa Afya nchini Marekani tayari wametahadharisha kuwa nchi hiyo inaweza kukabiliwa na kiwango hatari cha maambukizi pindi wimbi la pili la mlipuko wa virusi vya corona utatokea msimu wa majira ya baridi.

Mkurugenzi wa kituo cha udhibiti wa magonjwa nchini humo amesema wamarekani wanapaswa kujitayarisha kwa awamu ya pili ya mlipuko wa COVID-19 na hali itakuwa mbaya zaidi iwapo itachanganyika na mlipuko wa mafuta makali.

Afisa huyo amewataka raia kuhakikisha wanapatiwa chanjo dhidi ya mafua kama njia ya kupunguza hatari ya kuandamwa na maradhi ya aina mbili yanayoshambulia mfumo wa kupumua.

Mataifa karibu yote duniani yangali yanapambana na virusi vya corona ambavyo hadi vimekwishawauwa watu 180,000 na kuambukiza wengine milioni 2.6.

Viongozi wa EU kujadili virusi vya corona

Brüssel PK von der Leyen / Michel Treffen Erdogan
Picha: Getty Images/AFP/J. Thys

Kanda ya Ulaya iliyoathiriwa zaidi na janga hilo imeshuhudia ongezeko la idadi ya vifo hadi 110,00 huku Italia taifa lililopata pigo kubwa limerikodi jumla ya vifo 25,000

Viongozi wa Umoja wa Ulaya leo wanataka na mkutano mwingine wa kilele kutathmini hasara iliyotokana na janga la virusi vya corona kwa chumi za kanda hiyo pamoja na maisha ya watu.

Mkutano huo utakaondeshwa kwa njia ya video unanuwia kuidhinisha mpango kabambe wa kufufua uchumi wakati mataifa ya Ulaya yameanza kuondoa vizuizi vilivyowekwa kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Viongozi 27 wa nchi wanachama wanatakiwa kukubiliana kuhusu hatua za matumizi pamoja kufanya mashauriano juu ya mkakati wa uokozi unaotarajiwa kutangazwa wiki zinazokuja.