1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wenyeji Gabon waifunga Tunisia na kuchukua usukani wa kundi C

1 Februari 2012

Bao lake mchezaji Pierre Emerick Aubameyanga ambalo liliipa ushindi Gabon dhidi ya Tunisia mjini Franceville hapo jana liliwapeleka wenyeji hao wa kombe la mataifa ya bara Afrika hadi kileleni mwa kundi C.

https://p.dw.com/p/13txi
Kipa wa Tunisia Rami Jeridi, kulia, ashindwa kulizuia bao kutoka kwa Pierre Eymerick Aubameyang wa Gabon, kushoto, kwenye mchuano wa jana wa kundi C
Kipa wa Tunisia Rami Jeridi, kulia, ashindwa kulizuia bao kutoka kwa Pierre Eymerick Aubameyang wa Gabon, kushoto, katika mchuano wa jana wa kundi CPicha: dapd

Matokeo hayo ya bao moja kwa nunge ulikuwa ushindi wa tatu kwa Gabon kutokana na mechi nyingi na unaipa pointi tisa, huku nao Tunisia ambao tayari walikuwa wamefuzu kwa awamu ya maondowano kabla ya mechi hiyo ya mwisho ya makundi, wakimaliza wa pili na pointi sita.

Morocco nao ambao waliwazaba Niger goli moja kwa sifuri katika mchuano mwingine wa kundi C uliochezwa hapo jana mjini Libreville, walimaliza mechi za makundi na alama tatu, huku Niger ikishindwa kusajili hata pointi moja.

Ghana mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu

Mjini Franceville timu zote mbili baina ya Gabon na Tunisia zilionekana kujizatiti ili kuushinda mchuano huo na kuepuka uwezekano wa kukutana na Ghana katika robo fainali, ambayo ni mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu katika dimba hilo. Aubemeyang, ambaye babake Pierre, alikuwa nahodha wa kikosi cha Gabon mnamo mwaka 1994 na akawa katika kikosi hicho miaka miwili baadaye, wakati walipoponea awamu ya makundi kwa mara ya kwanza, aliandaliwa pasi safi kutoka kwake Daniel Cousin katika dakika ya 62.

Mshambuliaji huyo wa klabu ya Ufaransa St Etienne aliusogeza mpira hadi katika eneo la hatari kabla ya kumchenga kipa na kuongeza idadi ya mabao yake kufika matatu katika dimba hilo, na kumfanya kuwa mfungaji bora pamoja na Manucho wa Angola, na Houcine Kharja wa Morocco.

Tunisia ambao waliingia katika mechi hiyo wakifahamu wazi kuwa wangefaa kushinda ili kumaliza juu ya Gabon, walifanya mashambulizi ya kutafuta mabao baada ya kunyukwa bao na Gabon, lakini hawakufanikiwa kutokana na ngome dhabiti ya ulinzi ya vijana wa Gabon.

Wachezaji wa Gabon wakisheherekea ushindi wao jana dhidi ya Tunisia
Wachezaji wa Gabon wakisheherekea ushindi wao jana dhidi ya TunisiaPicha: dapd

Gabon watatoana kijasho na nambari mbili wa kundi D siku ya jumapili katika mchuano wa robo fainali mjini Libreville huku Tunisia ikikabana koo na mshindi wa kundi hilo la D katika mchuano mwingine wa robo fainali siku ya jumapili mjini Franceville.

Idadi ndogo ya mashabiki viwanjani

Katika mchuano mwingine wa jana mjini Libreville, kocha wa Morocco Eric Gerets alikifanyia mabadiliko mengi kikosi chake, ambacho tayari kilikuwa kimebanduliwa nje ya dimba hilo kabla ya mchuano huo. Ijapokuwa waandalizi walipeana tiketi za bila malipo kwa mchuano huo, ni karibu mashabiki 1,000 tu waliojitokeza katika uga wa stade de L'Amitie ambao una uwezo wa kuwa na mashabiki 40,000 walitazama mchuano wa kufedhehesha, ambao Morocco ilitawala lakini ikashindwa kuona lango hadi dakika ya 79 wakati Younes Belhanda alipotikisa wavu.

Shangwe kubwa zilisikika uwanjani baada ya kutangazwa kuwa Gabon ilikuwa imeshinda mjini Franceville. Kocha wa Morocco Eric Gerets alisema alifurahishwa kuwaona vijana wake wakionyesha mchezo bora na kusajili ushindi baada ya kushindwa michuano miwili ya mwanzo.

Awali Cote d'Ivoire na Sudan zilifuzu kwa raundi ya nane za mwisho katika kundi B huku wenyeji wengine wa dimba hilo Guinea ya Ikweta na Zambia wakifuzu kwa awamu hiyo katika kundi A.

Nafasi mbili za mwisho za robo fainali kuamuliwa leo

Nafasi mbili zinazosalia za robo fainali zitaamuliwa katika michuano ya hii leo ya kundi D mjini Franceville na Libreville. Botswana watakabana koo na Mali huku nao Ghana wakipambana na Guinea.

Mmoja wa mashabiki wa soka katika dimba la mataifa ya bara Afrika
Mmoja wa mashabiki wa soka katika dimba la mataifa ya bara AfrikaPicha: AP

Wakati huo huo, shirikisho la soka nchini Zambia – FAZ limethibitisha kuwa kiungo wa kati Clifford Mulenga amerejeshwa nyumbani kutoka kwa mashindano hayo baada ya kukiuka kanuni iliyowazuia kuwa nje kwa wakati uliowekewa kikosi chao. Msemaji wa FAZ amesema Mulenga na wenzake watatu walikwenda kusheherekea ushindi wao dhidi ya Guinea ya Ikweta. Lakini walirejea hotelini wakiwa wamechelewa na wakati wenzake walipoomba msamaha, Mulenga alikataa. Zambia inaongoza kundi A na itakutana na Sudan katika mchuano wa jumamosi wa robo fainali.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef