1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Tanzania achukia kuwa ombaomba

19 Julai 2017

Waziri wa Fedha wa Tanzania, Phillip Mpango, anasema anaipenda kazi yake lakini kinachomchukiza ni kuomba nchi nyingine kulisaidia taifa hilo lenye utajiri wa rasilimali. Tahariri ya Anaclet Rwegayura.

https://p.dw.com/p/2gon3
Waziri wa Fedha Tanzania Philip Mpango
Picha: DW/S. Khamis

Inapobidi afanye majadiliano na wahisani kuhusu misaada ya maendeleo ya nchi, waziri huyo anaeleza kuwa anajisikia vibaya, ingawa ujasiri wake kwa kazi hiyo hautiliwi mashaka.

"Hakuna jambo linalodhalilisha mwakilishi wa serikali kwenda kuombaomba msaada kwa wahisani,” Bw. Mpango alisema hivi karibuni alipotembelea ofisi ya Mamlaka ya Kodi Tanzania jijini Dar es Salaam, ambapo kulikuwa na foleni kubwa ya watu walifika kulipa kodi ya majengo.

Ujumbe wa waziri kwa walipakodi ulikuwa wazi kabisa. Serikali ya Tanzania ina shauku kubwa kuondokana na dalili ya utegemezi kwa wahisani. Kila mwaka, bila kujali ni nani alishika uwaziri wa fedha katika miaka 57 ya uhuru wan chi hii, bajeti ya serikali huninginizwa kwenye nyuzi za wahisani.

Katika hali hii serikali itawezaje kupanga ajenda ya maendeleo inayolenga watu wake? Hapana shaka ajenda hiyo itadhohofishwa kwa masharti ya ama moja kwa moja au vinginevyo, yanayowekwa na mshika mkoba.

Mwishowe matokeo yake yatapelekea utawala wenye kuwiwa madeni mahali ambapo hapatamaniki na shinikizo lisilolegea katika majadiliano ya kupanga madeni. Jambo kama hilo litamvunja moyo zaidi Bw. Mpango.

Wabunge Tanzanaia
Wabunge TanzanaiaPicha: DW/S. Khamis

Agenda ya maendeleo inayolenga wananchi ili ifanikiwe lazima isitegemee sadaka za wafadhili. Fedha za kutekeleza mipango ya maendeleo ya Tanzania hapana budi zikusanywe kutokana na kodi na watu lazima watambue wajibu wao katika kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.

Ili kukabiliana na changamoto hii, serikali ya Rais John Pombe Magufuli imekuja na mikakati mipya na kuimarisha taratibu za zamani kuongeza mapato yake. Ingawa njia hizo hazijapimwa na muda, zinaelekea kuleta ongezeko la mapato.

Haijawahi kutokea Watanzania wa mijini kujitokeza kwa wingi kiasi hicho kulipa kodi ya majengo kama mwaka. Imebidi serikali iongeze muda wa kulipa hadi mwisho wa Julai 2017 ili kila mtu alipe kodi yake. Lakini kwa nini haikuwa hivyo miaka iliyopita?

Wengi wamesema kuwa wamelipa kodi kuepukana na adha ya kupelekwa mahakamani na kutozwa faini. Lakini, wengine wanaeleza kuwa wameridhishwa na umakini wa serikali katika matumizi ya fedha za umma kwa sababu huko nyuma serikali za mitaa zilifanya ubadhirifu na fedha hizo.

Akiwa na shauku ya kuinua uchumi na hali za maisha ya wananchi, Rais Magufuli amewaonya maafisa wa serikali wilayani na mikoani kuzingatia kanuni za matumizi ya fedha za umma kama wanataka kubaki na kazi zao.

Maamuzi yake na hatua anazochukua kuendeleza uchumi wa Tanzania zinanifanya nione kuwa siyo tena wakati wa hadithi ya zamani kwamba, "kile nchi maskini zilichopoteza, nchi zilizoendelea zikafaidi.” Lazima ushindi uwe kwa wote sasa.

Rais wa Tanzania John Magufuli
Rais wa Tanzania John MagufuliPicha: picture-alliance/Anadolu Agency/B.E. Gurun

Sera za Magufuli kurekebisha uchumi ni za wakati unaofaa, na sasa, kwa mfano, zinaonyesha maendeleo ya kuleta haki kati ya serikali na wawekezaji katika sekta ya madini. Alipoanza kuelekeza sekta hiyo iongeze thamani kabla ya kusafirisha madini kuuzwa nchi za nje, baadhi ya wadau walikuwa na mashaka.

Wengine walieleza hofu yao kwamba wafanyakazi wa migodini wangepoteza kibarua kama wawekezaji wageni wanaopinga sera hizo wangefunga shughuli zao na kuondoka Tanzania. Wengine zaidi walisema kuwa joto la mbinu zake lilikuwa limepita kiasi.

 Hawakutambua kwamba alikuwa na mkakati maalum alioweka kwa uangalifu. Lakini  baada ya kuelewa, kampuni za kigeni zilianza kutangaza moja baada ya nyingine kuwa zilikuwa tayari kulipa asilimia 6 ya mrabaha iliyowekwa kwenye metali zote chini ya sheria mpya ya Tanzania kuhusu mali asili na majadiliano yawe baadaye.

 Rais Magufuli anaondoa vikwazo vyote kuifikisha Tanzania kwenye ngazi ya nchi za uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kujenga viwanda na kuboresha tija katika kila sekta. Wawekezaji hawana sababu kuhofu ili mradi wanafanya biashara safi bila kupitisha kitu mlango wa nyuma.

Kwa Waziri Mpango, ningemshauri kwamba, ‘kama unaipenda kazi yako, hakuna tatizo'. Kazi ni ngumu. Lakini jinsi wananchi wanavyounga mkono wito wa kulipa kodi, wanunuzi na wateja wa huduma mbalimbali wanavyodai risiti za EFD kwa kila shilingi, ni ishara ya ushindi.

Mwandishi: Anaclet Rwegayura/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef