1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa fedha wa Uingereza kukutana na wenzake wa EU

9 Desemba 2024

Waziri wa Fedha wa Uingereza Rachel Reeves atashiriki siku ya Jumatatu katika mkutano na wenzake wa Umoja wa UIaya mjini Brussels, Ubelgiji.

https://p.dw.com/p/4ntpt
Waziri wa Fedha wa Uingereza Rachel Reeves
Waziri wa Fedha wa Uingereza Rachel ReevesPicha: Jack Hill/The Times Ceo Summit/PA Media/dpa/picture alliance

Mkutano huo unalenga kujenga mahusiano ya kibiashara chini ya misingi ya kuaminiana na kuheshimiana kati ya pande hizo mbili na utakuwa wa kwanza tangu Uingereza ilipojiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, hatua inayofahamika kama Brexit.

Waziri huyo wa Uingereza anatarajia kusisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vya biashara, kuunda fursa za uwekezaji na kupiga jeki mahusiano ya  biashara kati ya Uingereza na mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Soma pia: Starmer: Vigumu kurejesha uhusiano na EU kama awali

Tangu ilipoingia madarakani mwezi Julai, serikali ya chama cha Labour inayoongozwa na Waziri Mkuu Keir Starmer imekuwa ikijaribu kufufua upya uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza, baada ya miaka mingi ya mvutano na chama cha Conservatives. Hata hivyo Uingereza imeeleza mara kadhaa kuwa haina nia ya kurejea ndani ya Umoja huo.