1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mariano Rajoy ameshindwa katika kura ya kutokuwa na imani

Shisia Wasilwa
1 Juni 2018

Waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ameshindwa katika kura ya kutokuwa na imani naye bungeni leo na kumpa nafasi kiongozi wa chama cha kisoshalisti Pedro Sanchez kuwa waziri mkuu ajaye.

https://p.dw.com/p/2ynX1
Spanien Madrid - Ministerpräsident Rajoy per Mistrauensvotum gestürzt
Picha: Reuters/P.-P. Marcou

Sanchez alishinda kwa  kura 180 dhidi ya 169 zilizopinga na  moja kujizuwia kupiga kura.

Rajoy  ameondolewa madarakani kutoka na kashfa ya ufisadi iliyokikumba chama chake cha Popular Party PP ambapo maafisa wa zamani wameshitakiwa kwa kuchukua rushwa ili kutoa kandarasi.

Kabla ya kura kupigwa Rajoy aliliambia bunge la nchi hiyo kuwa anajivunia rekodi yake kama waziri mkuu wa taifa hilo, akimpongeza mpinzani wake Sanchez na wabunge wa chama tawala cha Popular Party- PP wakimpigia makofi na kusimama kumuonesha heshima zao.

Rajoy  alisema  ilikuwa ni  fahari kwake  kuiacha Uhispania katika hali nzuri kuliko alivyoikuta na kuwashukuru Wahispania na kuwatakia kila la kheri.

"Imekuwa ni fahari kuwa Waziri Mkuu wa Uhispania. Ni fahari kuweza kuondoka na kuacha Uhispania kuwa bora kuliko jinsi nilivoipata." 

Sanchez hatakubali Catolonia kujitenga 

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Kisosholisti Pedro Sanchez aliliambia bunge  kabla ya matokeo kwamba   leo wanaandika historia kuhusu demokrasia ya taifa hilo. Lakini mbunge wa chama cha PP Rafael Hanando amemwambia Sanchez kuwa atakuwa waziri mkuu wa Uhispania kupitia mlango wa nyuma kwasababu alishidwa katika uchaguzi mwaka 2015 na 2016.

Kuondoka kwa Rajoy baada ya miaka sita kama Waziri mkuu kutaliweka taifa hilo lenye uchumi wa nne kwa ukubwa katika Umoja wa Ulaya katika hali ya wasiwasi na kisiasa, Italia inapojikwamua kutoka kwenye mzozo. 

Pedro Sanchez kiongozi wa PSOE
Pedro Sanchez Kiongozo wa PSOEPicha: Getty Images/P. Blazques Dominguez

Wawekezaji wengi hawaoni hatari ya kuwekeza nchini Uhispania kama ilivyo Italia kwani Sanchez mwenyewe anaiunga mkono Ulaya ambapo viongozi wengi wa vyama vya miungano wameibua masuala kuhusu nia zao za kuunga mkono sarafu ya euro.

Vyama viwili vinavyounga mkono uhuru wa Catalonia pamoja na kile cha mrengo wa kushoto cha Podemos pia vilisema  tangu awali vitamuunga mkono Sanchez. Sanchez ameahidi  kuanzisha mazungumzo na Wakatolonia, lakini akasema hatuwapa nafasi ya kujitenga.

Baada ya kura Sanchez anatarajiwa kuapishwa wikendi hii na kuteua baraza lake la mawaziri. Hata hivyo akiwa na viti 84 kati ya 350 vya bunge, serikali yake itakuwa na wakati mgumu wa kupitisha sheria.

Uchaguzi mkuu  wa Uhispania umepangwa kufanyika katikati ya mwaka 2020 na haijabainika iwapo Sanchez ataitisha uchaguzi mkuu wa  mapema kabla ya  wakati.

Wadadisi wengi wanasema kuwa huenda akasubiri hadi kufanyika kwa uchaguzi wa  Ulaya,  wa mitaa na wa majimbo  mwezi Mei mwaka ujao.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Reuters, Dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman