Wazimbabwe waandamana kupinga kupanda kwa bei ya mafuta
14 Januari 2019Katika baadhi ya maeneo mjini Harare na miji mengine waandamani walichoma matairi na kuziba barabara baada ya muungano wa vyama vya wafanyakazi kuitisha maandamano. Polisi walliwafyatulia risasi za moto waandamanaji katika eneo la Epworth, lililoko umbali wa kilomita 15 kutoka mjini Harare.
Baadhi ya watu walijeruhiwa na wengine kukamatwa japokuwa idadi yao bado haijawekwa wazi. Baadhi ya waandamanaji wanasema wamechanganyikiwa na kile kinachotokea nchini mwao.
Vurugu nchini Zimbabwe zimetokea siku moja baada ya rais Emmerson Mnangagwa kupandisha zaidi ya mara mbili bei ya mafuta kufuatia ukosefu wa bidhaa hiyo.
Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini humo uliitisha maandamano ya siku tatu kufuatia tamko hilo la rais Mnangagwa la kupandisha bei ya mafuta huku biashara nyingi na shule zikifungwa hii leo. Msemaji wa muungano huo Peter Mutasa amesema hatua ya serikali inaonyesha kutoguswa na kutojali kuhusu mwananchi masikini ambaye tayari amelemewa na majukumu chungu nzima.
Hata hivyo serikali imejibu maandamano kwa kuwatawanya polisi wa kupambana na ghasia huku helikopta za kijeshi zikionekana angani.
Upinzani wasema wananchi wana haki ya kuandamana
Huku hayo yakiarifiwa kiongozi wa chama cha upinzani MDC Nelson Chamisa, amesema kupitia mtandao wake wa kijamii wa twitter, kwamba maafisa wa usalama wanapaswa kujizuwiya na kuwaacha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kuandamana kwa amani.
Ukosefu wa pesa taslimu Zimbabwe umeutumbukiza uchumi wa taifa hilo la Kusini mwa Africa katika matatizo makubwa hali inayotishia vurugu zaidi na kudhoofisha juhudi za rais Mnangagwa za kurejesha uekezaji wa kigeni uliotengwa na mtangulizi wake Robert Mugabe.
Maisha ya kila siku yanazidi kuwa magumu huku bei za bidhaa za msingi zikipanda na usambazaji wa madawa ukipungua. Misafara mirefu inaonekana barabarani na katika vituo vya mafuta na wanajeshi wakidhibiti vurugu zinazoweza kutokea wakati wakaazi waking'ang'ania mafuta.
Habari ya kupanda kwa bei hiyo ya mafuta kwa asilimia 150 ilipokelewa kwa mshituko nchini Zimbabwe ambapo idadi ya wasio na ajira imefikia asilimia 80. Huku Ghasia zikiendelea Rais Emmerson Mnangagwa ameelekea Ulaya kuhudhuria kongamano la kiuchumi mjini Davos, Uswisi akijaribu kuwashawishi wawekezaji wa Kigeni kurudi kuwekeza Zimbabwe.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga