1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli aombolezwa Zanzibar kwa hisia mchanganyiko

Salma Said18 Machi 2021

Wakaazi wa visiwani Zanzibar wamezipata taarifa za kifo cha Rais John Magufuli, mwezi mmoja kamili baada ya habari za cha kiongozi mwingine muhimu, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar.

https://p.dw.com/p/3qnRt
Tansania - Präsident John Magufuli
Picha: picture alliance/AA/M. Mukami

Hayati Magufuli anaombolezwa visiwani humo kwa hisia mchanganyiko.

Ni Jumatano ya tarehe 17 ambayo haitasahaulika vichwani mwa watanzania kwa kupokea taarifa hizo za msiba ambazo zimeanza kusambaa tokea usiku wa saa tano lakini wazanzibari wengi wamepata taarifa asubuhi huku baadhi ya shughuli za serikali zikiakhirishwa na watu kujikusanya kwa makundi kuzungumzia suala hilo.

Kwa waliokuwa wakimpenda Rais Magufuli walizungumza kwa hisia za kumpoteza kiongozi huyo na kusema kwamba amewacha pengo kubwa kwa siasa za Tanzania ikiwa ni pamoja na kuunga mkono maridhiano ya Zanzibar na ujasiri wake wa kuongoza nchi.

Kathrine Peter nao ni Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na msiba huo kuupokea kwa kuwaduwaza lakini wanamshukuru Magufuli kwa kuwa amewafunza namna gani Tanzania ilivyo na rasilimali za kutosha.

“Nasema jambo lililotupata wanaCCM tumeduwaa lakini nasema na tumshukuru Mungu kwa kila jambo na dini zetu zote zinasema hivyo tushukuru kwa kila jambo” amesema Cathrine.

Kwa upande wengine waliokuwa wakimkosoa wanaona kuwa ni fursa muhimu ya kurejesha uhuru wa demokrasia na uhuru wa habari ambao uliminywa katika kipindi chake chote cha uongozi. Salum Vuai ni mmoja wa wachambuzi wa wa masuala ya kijamii.

Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu kupoteza sifa za uchaguzi au maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano.