1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wavenezuela wapiga kura isiyo rasmi

Sylvia Mwehozi
17 Julai 2017

Upinzani nchini Venezuela umedai kuwa Wavenezuela zaidi ya theluthi moja walijitokeza siku ya Jumapili(16.07.2017)katika kura ya maoni isiyo rasmi iliyoandaliwa na upinzani huku watu wawili wakiripotiwa kupoteza maisha.

https://p.dw.com/p/2geRt
Venezuela Caracas Referendum
Picha: Picture Alliance/AP Photo/A. Cubillos

Spika  wa bunge la nchi hiyo Julio Borges ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa watu zaidi ya milioni 7.2 walijitokeza jana katika kura hiyo isiyo rasmi, na kusema mwitikio huo ni ishara ya wazi ya kukatiliwa kwa rais Nicolas maduro.

Katika kura hiyo ya jumapili, baadhi ya raia milioni 19 wa Venezuela walitakiwa  kuupinga mpango wa rais Maduro wa kuchagua bunge maalumu litakaloandika tena katiba ya taifa hilo la Amerika ya kusini .

Waandaaji wanasema wapiga kura wengi walioshiriki katika kura hiyo ya maoni, ambayo imeitishwa na upinzani na ambayo inakatiliwa na serikali, kwamba waliukataa mpango huo wa Maduro katika sanduku la kura. Hata hivyo hapajakuwa na matokeo rasmi ya kura hiyo ya maoni hadi kufikia Jumatatu asubuhi.

Venezuela Symbolisches Referendum gegen Maduro
Raia wa Venezuela wakisubiria kupiga kura siku ya jumapiliPicha: Getty Images/AFP/J. Barreto

Watu wawili wameuawa wakati wa vurugu zilizozuka wakati wa mchakato wa upigaji kura. Watu wenye silaha walivamia kituo cha kupigia kura kilichopo karibu na kanisa mjini Catia, kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Caracas kwa mujibu wa Carlos Ocariz, msemaji wa upinzani.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti  kuwa kiasi ya watu 500 waliomba hifadhi katika kanisa wakati wa shambulio hilo akiwemo Kadinali wa kanisa Katoliki Jorge Urosa. Kiongozi wa upinzani Henrique Capriles amesema watu hao waliokuwa na silaha waliwashambulia waandamanaji wakiwa katika pikipiki. Katika ukurasa wake wa Twitter, amemshutumu rais Nicolas Maduro na "utawala wake mbaya" kwa kuwatuma "wajumbe wake" kuishambulia Catia.

Taarifa za vyombo vya habari pia zinasema wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wanaojulikana kama "colectivos" waliwafyatulia risasi wafuasi wa upinzani.

Venezuela Caracas Referendum Henrique Capriles
Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Henrique Capriles akipiga kuraPicha: Picture Alliance/AP Photo/A. Cubillos

Kura hiyo ya maoni iliitishwa na bunge linalodhibitiwa na upinzani, ambalo linaamini kutuma ujumbe wa  wazi kwa serikali ya kisosholisti kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura waliojitokeza.

Taifa hilo lenye utajiri wa mafuta linakabiliwa na mgogoro mbaya wa kiuchumi, ikiwemo uhaba wa bidhaa muhimu pamoja na kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei. Zaidi ya watu 90 wameuwawa katika maandamano ya kuipinga serikali ambayo yametokea angalau kila siku kuanzia mwezi Aprili.

Maduro ambaye amekataa kuachia ngazi, pia ameitisha kura yake baadae mwezi huu ili kuchagua bunge maalumu. Upinzani unaona mipango yake ya kubadili katiba kama jaribio la kuimarisha mamlaka yake.  

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa

Mhariri: Saumu Yusuf