1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watunisia waunga mkono Katiba mpya katika kura ya maoni

Sylvia Mwehozi
26 Julai 2022

Raia wa Tunisia walioshiriki kura ya maoni siku ya Jumatatu wamepiga kwa wingi kura ya "ndiyo" kuunga mkono katiba mpya katika matokeo ya awali, hatua inayompa mamlaka zaid rais Kais Saied.

https://p.dw.com/p/4Edve
Tunesien Tunis | Referendum zur Verfassung
Picha: ZOUBEIR SOUISSI/REUTERS

Kura hiyo iliyofanyika ikiwa ni mwaka mmoja kamili tangu rais Saied alipoivunja serikali na kusimamisha bunge, imeshuhudia asilimia 27 ya wapiga kura milioni 9.3 waliojiandikisha wakishiriki mchakato huo, kulingana na tume ya uchaguzi ya Tunisia.

Matokeo ya awali yaliyotolewa na taasisi ya Sigma Conseil yameonesha kuwa asilimia 93 ya wale waliopiga kura wameunga mkono Katiba mpya.Tunisia kuunda kamati ya kuandika katiba mpya

Ushiriki wa raia katika kura ya Jumatatu ulikuwa ukitizamwa kama kipimo cha umaarufu wa Saied baada ya mwaka mmoja wa kupanua mamlaka yake. Baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa, wafuasi wake walimiminika mitaani wakishangilia na kuonyesha uungaji mkono wa rais huyo.

Tunesien | Proteste gegen das Referendum von Präsident Kais Saied über eine neue Verfassung
Maandamano ya kupinga uchaguzi wa kura ya maoniPicha: Zoubeir Souissi/REUTERS

Mara baada ya kupiga kura Rais Saied alisema kuwa Tunisia inakabiliwa na "chaguo la kihistoria", akiongeza kuwa taifa hilo litastawi na kusonga mbele. 

"Tutajenga pamoja kwa mikono yetu, mawazo na azma yetu. Tutajenga Mungu akipenda jamhuri mpya, tutajenga jamhuri mpya yenye msingi wa uhuru wa kweli na haki ya kweli na utu wa taifa kwa sababu hakuna utu kwa mataifa isipokuwa kwa heshima ya raia wake," alisema Saied.

Baadae katika mahojiano yaliyorushwa na kituo cha Al jazeera hii leo, Rais Saied amenukuliwa akisema kwamba uamuzi wake wa kwanza baada ya kura ya maoni, utakuwa ni kubadili sheria ya uchaguzi. Ameongeza kuwa sheria hiyo itabadili mfumo wa zamani wa uchaguzi ambao maafisa waliochaguliwa hawafuati matakwa ya wapiga kura.

Hatua za rais Saied dhidi ya mfumo ulioibuka baada ya kupinduliwa kwa dikteta Zine El Abidine Ben Ali mwaka 2011 zilipokelewa kwa shangwe na raia wengi wa Tunisia ambao walikuwa wamechoshwa na mfumuko mkubwa wa bei, ukosefu wa ajira na mizozo ya kisiasa.Muungano wenye nguvu Tunisia umekosoa mpango wa Rais Saied

Vyama vya upinzani vilisusia kura hiyo na vinamtuhumu Saied kwa kuanzisha utawala wa Kiimla katika taifa ambalo ni chimbuko la vuguvugu la maandamano ya uarabuni. Katiba hiyo mpya inaondoa katiba ya mwaka 2014 ambayo ilipatikana baada ya maelewano kati ya vikosi vinavyoegemea Uislamu na vile vya kawaida. Wafuasi wa Saied wanalaumu matokeo ya mfumo wa urais na ubunge na chama chenye ushawishi wa Kiislamu cha Ennahdha kwa miaka mingi ya migogoro ya kisiasa na ufisadi.

Saied, profesa wa sheria mwenye umri wa miaka 64, alishinda kwa kishindo uchaguzi wa urais wa mwaka 2019,  akijijenga jina kama mwanasiasa asiyetikiswa na ufisadi.