1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Watu wapatao 150 wafa katika mkanyagano Korea Kusini

Sylvia Mwehozi
30 Oktoba 2022

Takribani watu 150 wamefariki dunia huko Korea Kusini katika mkanyagano uliotokea wakati wa sherehe za Halloween mjini Seoul usiku wa Jumamosi.

https://p.dw.com/p/4IqDm
Südkorea Halloween Massenpanik
Picha: Chung Sung-Jun/AFP/Getty Images

Mkasa huo umetokea wakati umati mkubwa wa vijana waliokuwa wakisherehekea sikukuu ya Halloween huko mjini Seoul kunaswa na kukandamizwa katika uchochoro mwembamba. Maafisa wanasema watu wengine 150 wamejeruhiwa katika mkasa huo mbaya kuwahi kutokea nchini Korea Kusini kwa miaka mingi.

Mkanyagano huo umetokea karibu na Hoteli ya Hamilton katika wilaya ya Itaewon ambayo ni maarufu kwa burudani za usiku huku idadi kubwa ya watu wakiwa wamekusanyika katika uchochoro mwembamba karibu na hoteli hiyo.

Sherehe hizo za Halloween zilikuwa ndio za kwanza kufanyika mjini Seoul ndani ya kipindi cha miaka mitatu baada ya serikali kuondoa vizuizi vya Covid-19. Wahanga wengi walikuwa wamevalia barakoa na mavazi maalum ya sherehe za Halloween.

Südkorea Halloween Massenpanik
Wahudumu wa uokozi katika eneo la mkasa wa mkanyaganoPicha: Lee Ji-eun/Yonhap/AP Photo/picture alliance

Mashahidi wameelezea matukio ya ghasia muda mfupi kabla ya kutokea mkanyagano, huku polisi waliokuwa wakifuatulia sherehe hizo za Halloween wakishindwa kudhibiti umati mkubwa wa watu. Kijana mmoja anayeitwa Monn Ju-Young amelieleza shirika la habari la Reuters kwamba "kulikuwa na dalili zote kwamba kutakuwa na tatizo kwenye uchochoro kabla ya tukio".

Mashuhuda wengine wameeleza jinsi walivyokuwa wakihaha kutoka katika umati uliokuwa umefurika, wakati watu wakirundikana juu ya wengine, na wahudumu wa afya waliozidiwa na idadi ya wahanga wakiomba usaidizi kwa wapita njia.Watu 174 wamekufa katika mkanyagano nchini Indonesia

Kwa mujibu wa maafisa wa zima moto watu waliendelea kumiminika kwenye uchochoro mwembamba ambao tayari ulikuwa umefurika ukuta hadi ukuta, wakati wengine waliokuwa juu ya barabara yenye mteremko wakianguka na kuwaangusha wengine.

Afisa wa idara ya Zimamoto Choi Seong-beom amesema "idadi kubwa ya majeruhi ilitokana na wengi kukanyagwa wakati wa sherehe za Halloween," akiongeza kwamba idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka.

Südkorea Halloween Massenpanik
Baadhi ya mabaki ya mavazi ya HalloweenPicha: Chung Sung-Jun/Getty Images

Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol ameamuru maafisa kupeleka timu za huduma ya kwanza na kuweka tayari vitanda hospitalini kwa walioathirika. Wakati huo huo, Meya wa Seoul Oh Se-hoon, ambaye alikuwa ziarani barani Ulaya, amelazimika kukatisha ziara yake, kulingana na shirika la habari la Korea Yonhap.

Mitandao ya Kijamii

Picha za kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha mamia ya watu wakiwa wamejazana kwenye kichochoro chembamba kilicho kwenye mteremko huku polisi na maafisa wa msaada wa dharura wakijaribu kuwavuta na kuwatoa. Picha nyingine zimeonesha matukio ya maafisa na raia wakiwapatia huduma ya kwanza watu wengi ambao walionekana kupoteza fahamu.

Tukio hilo limetokea katika wilaya ya Itaewon mjini Seoul ambayo ni maarufu kwa burudani za usiku na kutembelewa zaidi na vijana na wageni huku ikiwa imesheheni migahawa na sehemu za burudani.Watu 29 wafa katika mkanyagano, Liberia

Viongozi wa ulimwengu watoa salamu za pole

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ametoa salamu za rambirambi kufuatia mkasa huo wa Korea Kusini, akisema kuwa "ni tukio la kutisha huko Seoul na imetushtua sisi sote."

Rais wa Marekani Joe Biden amesema Marekani "inasimama pamoja" na Korea Kusini kufuatia mkanyagano uliosababisha vifo vya watu kwenye sherehe za Halloween katika mji mkuu wa nchi hiyo ambao umeua takriban watu 150.