1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kadhaa waripotiwa kuambukizwa Mpox Afrika Kusini

19 Agosti 2024

Idadi ya watu walioripotiwa kuwa na ugonjwa wa Mpox nchini Afrika Kusini, imeongezeka na kufika wagonjwa 24 na vifo vitatu vimerekodiwa hadi sasa.

https://p.dw.com/p/4jcYo
Mlipuko wa Homa ya Nyani yatajwa kuwa dharura ya afya ya umma
Tayari kituo cha kudhibiti na kuzuwia magongwa barani Afrika CDC, kimesema mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani au mpox, ni dharura ya afya ya umma.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Kesi 12 kati ya hizo ziliripotiwa jimboni Gauteng, 11 KwaZulu-Natal, 1 huko Western Cape na tayari watu 19 wameshapona huku wagonjwa wawili wakiendelea kutengwa nyumbani.

Msemaji wa wizara ya Afya Foster Mahal amesema serikali imeanza kudhibiti ugonjwa huo kikamilifu, kwa kuongeza uchunguzi mipakani na amekiri kwamba kutakuwa na ongezeko la wagonjwa wa Mpox siku hadi siku nchini Afrika Kusini.

Wananchi wametakiwa kutekeleza wajibu wao na kuunga mkono juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo, ili kuzuia kuenea kwa homa ya nyani kwa kudumisha usafi wakati wote.

Wiki iliyopita, kituo cha kudhibiti na kuzuwia magongwa barani Afrika CDC, kilisema mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani au mpox, kuwa dharura ya afya ya umma.