1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 76 wauawa kwenye mlipuko wa bomu Mogadishu

28 Desemba 2019

Bomu la kutegwa ndani ya gari limelipuka leo asubuhi katika kituo kimoja cha ukaguzi wa usalama chenye shughuli nyingi katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, na kuwauwa karibu watu 76

https://p.dw.com/p/3VQfu
Somalia Mogadischu Autobombe an Checkpoint
Picha: Reuters/F. Omar

Bomu la kutegwa ndani ya gari limelipuka leo asubuhi katika kituo kimoja cha ukaguzi wa usalama chenye shughuli nyingi katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, na kuwauwa karibu watu 76.

Mkuu wa hospitali ya Medina Mohamed Yusuf amethibitisha idadi hiyo akisema watu wengine 70 wamerujiwa. Awali, msemaji wa serikali Ismail Mukhtar alisema idadi hiyo huenda ikaongezeka kwa sababu zaidi ya watu 60 wamekimbizwa katika hospitali mbalimbali. Limekuwa mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi kutokea katika siku za karibuni mjini Mogadishu.

Kapteni Mohamed Hussein amesema mlipuko huo ulikilenga kituo cha kukusanya kodi wakati wa pilikapilika za asubuhi wakati wakazi wakirejea kazini baada ya mapumziko ya mwishoni mwa juma. Hakujatolewa taarifa yoyote kuhusu aliyehusika na shambulizi hilo. Kundi la itikadi kali la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda aghalabu hufanya mashambulizi ya aina hiyo.