Watu 65 wauawa, mapigano yakiongezeka Sudan
4 Februari 2025Kwa mujibu wa vyanzo viwili vya kitabibu, katika jimbo la Kordofan Kusini, takriban watu 40 wameuwawa na wengine 70 wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi kwenye mji mkuu wa jimbo la Kadugli.
Mji huo, unaodhibitiwa na jeshi la Sudan, ulilengwa katika shambulio ambalo Gavana Mohamed Ibrahim alililaumu kundi la Sudan People's Liberation Movement-North (SPLM-N), linaloongozwa na Abdel Aziz al-Hilu.
Soma pia: Shambulio dhidi ya soko Sudan lauwa watu 54 na kujeruhi 150
Aidha, gavana huyo amesema kwamba shambulizi hilo lililenga kudhoofisha eneo hilo, akiapa kuondoa "vikosi vya waasi" katika milima inayozunguka Kadugli. Katika muda wote wa vita hivyo, wapiganaji wa SPLM-N wamekabiliana na jeshi la Sudan na hata wanamgambo wa RSF katika maeneo tofauti ya jimbo la Kordofan Kusini.
Mapigano makali pia yalishuhudiwa katika eneo kubwa la magharibi mwa Darfur, mashambulizi ya anga ya kijeshi yaliulenga mji mkuu wa Darfur Kusini, Nyala, na kuwauwa watu 25 na kuwajeruhi wengine 63.
Daglo awapa motisha wapiganaji wake
Kulingana na shahidi mmoja katika eneo hilo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, shambulio hilo lilipiga Wilaya ya Nyala, eneo lililo chini ya udhibiti wa wanamgambo wa RSF.
Katika taarifa RSF imeshutumu jeshi kwa kutumia mabomu dhidi ya raia katika vitongoji kadhaa huko Nyala.
Soma pia: UN yaonya kuhusu mashambulizi ya kulipiza kisasi Sudan
Kiongozi wa wanamgambo RSF, Mohamed Hamdan Daglo ameapa kufukuza jeshi kutoka mji wa Khartoum.
"Endeleeni kusonga mbele na mema yatawajia, Mungu akipenda. Msizingatie kusonga kwao kwenye mtaa wa al-Inqaz au mtaa wa al-Maouna au kwenye Kamandi Kuu. Hawatofurahia Kamandi Kuu kwa muda mrefu."
"Ninawatolea wito mfikirie ni nini tutakachokidhibiti, sio juu ya kile walichokidhibiti. Hapana. Tutachukua nini? Lazima tusonge mbele, lazima tuangalie mbele."
Wakati jeshi la Sudan likisonga mbele katika mji mkuu, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alielezea wasiwasi wake kutokana na ripoti za mauaji ya raia huko Khartoum Kaskazini, yanayodaiwa kufanywa na wapiganaji na wanamgambo wanaoshirikiana na jeshi.
Soma pia: Umoja wa Mataifa washtushwa na kiwango cha mauaji ya raia Sudan
Wanamgambo wa RSF na jeshi la Sudan wamekuwa wakishutumiwa mara kwa mara kwa kuwalenga raia na kuyashambulia kwa makombora maeneo ya makazi.