1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroLebanon

Mzozo wa Israel na Hezbollah wapamba moto

24 Septemba 2024

Israel imezishambulia ngome za kundi la Hezbollah kusini mwa Lebanon huku Hezbollah kwa upande wao ikivishambulia vituo vya kijeshi kaskazini mwa Israel.

https://p.dw.com/p/4l0vY
Israel | Kiryat  Bialik | Mzozo | Lebanon
Timu ya uokoaji ikizima moto kufuatia shambulio la roketi kutoka Lebanon katikati ya uhasama kati ya Hezbollah na Israel eneo la Kiryat Bialik, Israel.Picha: Shir Torem/REUTERS

Hali hiyo inaongeza hofu ya kutokea vita kamili kati ya Israel na Hezbollah wakati Lebanon ikitangaza vifo vya zaidi ya watu 490 wakiwemo watoto 35 vilivyotokea kufuatia mashambulizi ya Israel.

Jeshi la Israel limesema limezishambulia ngome kadhaa za kundi la wanamgambo wa Hezbollah usiku wa kuamkia leo huku makumi kwa maelfu ya watu kusini mwa Lebanon wakikimbilia usalama wao.

Soma pia:  Mashambulizi ya Israel yauwa zaidi ya watu 270 Lebanon

Ama kwa upande wa Hezbollah, kundi hilo linaloungwa mkono na Iran limeeleza kuwa limevishambulia vituo vya jeshi la Israel kikiwemo kiwanda cha kutengeneza silaha.

Kundi hilo limesema limefanya mashambulizi hayo kwa kutumia roketi aina ya Fadi saa kumi leo alfajiri. Hezbollah imeongeza kuwa, imeushambulia pia uwanja wa ndege wa Megiddo karibu na mji wa Afula kaskazini mwa Israel.

Baada ya Hamas, Israel yaigeukia Hezbollah

Karibu mwaka mmoja wa vita kati yake na Hamas katika ukanda wa Gaza, Israel sasa inaonekana kubadili mkondo na sasa nguvu zao wamezielekeza kwenye mpaka wa kaskazini ambapo kundi la Hezbollah limekuwa likirusha makombora kuelekea Israel.

Ofisi ya waziri mkuu wa muda wa Lebanon Najib Mikati imesema kiongozi huyo atasafiri kuelekea New York, Marekani ambapo kunafanyika mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwa kile alichokiita "kufanya mazungumzo” na viongozi wakuu wa mataifa mbalimbali duniani kufuatia wimbi la mashambulizi ya anga ya Israel nchini Lebanon.

Vita hivyo vimeongeza hofu kuwa Marekani ambayo ni mshirika wa karibu wa Israel na Iran, inayoliunga mkono kundi la Hezbollah, zinaweza kutumbukia kwenye mzozo huo.

Lebanon | Sidon | Mzozo kati ya Hezbollah na Israel
Raia wa Lebanon waliokimbilia nyumba zao kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel kwenye barabara kuu inayounganisha mji wa Beirut katika mji wa bandari wa Sidon.Picha: Mohammed Zaatari/AP Photo/picture alliance

Mamia ya watu kutoka kusini mwa Lebanon wameonekana kupakia mizigo yao kwenye malori wakizihama nyumba zao na kutafuta sehemu salama. Msongamano mkubwa wa magari umeshuhudiwa katika barabara kuu ya kuelekea upande wa kaskazini.

Waziri wa Lebanon anayeshughulikia masuala ya dharura Nasser Yassin ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, kambi 89 za muda zenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya watu 26,000 zimetengwa kwa ajili ya kuwahudumia maelfu ya watu wanaokimbia makaazi yao kutoka kile alichokiita "ukatili wa Israel."

Soma pia: UN yaonya juu ya janga kubwa katika kanda ya Mashariki ya Kati 

Mousa Youffef, ni mkurugenzi wa matibabu katika hospitali kusini mwa Lebanon.

"Ni mauaji dhidi ya raia wasiokuwa na hatia na wala sio mashambulizi ya kijeshi kama wanavyodai Israel. Asilimia 90 ya waliojeruhiwa ni Watoto, majeraha yao ni pamoja na kuchomeka na kuvunjika viungo vya mwili. Ni hali ya kutisha na inaonyesha hali ya kutojali iliyopo sasa.”

Urusi yaeleza wasiwasi juu ya hali nchini Lebanon

Wizara ya afya ya Lebanon imesema watu wasiopungua 492 wameuawa wakiwemo watoto 35 na wengine wapatao 1,645 wamejeruhiwa. Afisa mmoja wa serikali amesema idadi hiyo ya vifo ni ya juu zaidi kuripotiwa kwa siku moja tangu kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1975 hadi 1990.

Wakati hayo yanaripotiwa, ikulu ya Kremlin imetahadharisha kuwa mashambulizi ya Israel nchini Lebanon yanatishia kuyumbisha eneo la Mashariki ya Kati na kwamba Urusi ina wasiwasi juu ya hali inayoendelea.

Soma pia:  Nasrallah aapa kulipa kisasi baada ya mashambulizi Lebanon

Naye Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema leo kundi la Hezbollah haliwezi kusimama pekee yake dhidi ya Israel.

Katika mahojiano na shirika la habari la Marekani CNN, kiongozi huyo wa Iran amesema "Hezbollah haiwezi kusimama pekee yake dhidi ya nchi ambayo inalindwa na kuungwa mkono na mataifa ya Magharibi na Marekani.