1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 45 wauwawa,Wabunge wapigwa mabomu ya machozi Nigeria

21 Novemba 2014

Kiasi cha watu 45 wameuawa kwenye eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria kutokana na mashambulizi ya Boko Haram, huku polisi kwenye mji mkuu Abuja ikitumia gesi ya machozi kuwazuia wabunge kuhudhuria kikao cha bunge

https://p.dw.com/p/1DrIi
Symbolbild Nigeria Polizei
Picha: imago/Xinhua

Kwa mujibu wa mashahidi, mashambulizi hayo yametokea kwenye kijiji cha Azaya Kura kilicho umbali wa kilomita 50 kutoka mji mkuu wa jimbo la Borno, Maiduguri. Chifu wa kijiji hicho, Mallam Bulama, ameliambia shirika la habari kwamba hadi kufikia jioni ya jana walikuwa wameshahisabu miili ya watu 45 baada ya kumalizika kwa mashambulizi hayo.

Jimbo la Borno limekuwa kitovu cha mashambulizi ya Boko Haram. Tarehe 26 mwezi uliopita, kundi hilo liliwateka nyara wasichana na wavulana 30, wengine wakiwa na umri wa hadi miaka 11, na takribani imekuwa ikivamia maeneo kadhaa ya jimbo hilo kila siku. Mwezi Machi watu 29 waliuawa baada ya kutumiwa vipeperushi kuwaonya kuwa wangelishambuliwa.

Mmoja wa wanavijiji waliofanikiwa kukimbia mashambulizi ya hapo Jumatano, Mohammed Bukar, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba washambuliaji waliharibu zaidi ya nusu ya nyumba za kijiji chao, wakazichoma moto pikipiki 50 na gari nne kabla ya kuondoka na chakula na wanyama kadhaa.

Anschlag in Maiduguri Nigeria Archiv Juli 2014
Mashambulizi ya Boko Haram katika mji wa Maiduguri.Picha: AFP/Getty Images

Hayo yakitokea, kwenye mji mkuu wa Nigeria, Abuja, polisi ilitumia mabomu ya machozi kujaribu kuwazuia wabunge wa upinzani, ikiwa ni pamoja na spika wa bunge, kushiriki kwenye kura muhimu juu ya pendekezo la Rais Goodluck Jonathan kuongeza muda wa hali ya hatari katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, ambako kundi la Boko Haram limekuwa likiendesha shughuli zake za kigaidi.

Katika vurugu hizo, wabunge waliokuwa wanapingana na ombi hilo walitaka badala yake ipigwe kura ya kumuondosha Rais Jonathan.

Nigerianischer Präsident Goodluck Jonathan 11.11.2014
Rais wa Nigeria Goodluck JonathanPicha: picture-alliance/AP

Chama kikuu cha upinzani nchini humo kimesema Rais huyo anakwenda kinyume na katiba kwa kuongeza muda wa hali ya dharura, na kwamba serikali yake imeshindwa kabisa kukabiliana na Boko Haram.

Spika wa Baraza la Seneti, David Mark, sasa amesitisha vikao vya bunge hadi hapo Jumanne. Spika huyo alitangaza kwamba polisi walitumia mabomu ya machozi kuzuia wabunge hao kukutana, ambapo wabunge hao walijaribu kulivunja lango la bunge kuingia ndani.

Licha ya mabomu hayo ya machozi, baadhi ya wabunge walifanikiwa kuingia ndani. Muda mchache kabla ya hapo, spika huyo alitangaza kuacha kumuunga mkono Rais Jonathan na kuungana na upande wa upinzani.

Mwandishi: Nyamiti Kayora/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef