1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Watu 400 wamekufa kwa njaa Ethiopia

31 Januari 2024

Takriban watu 400 wamekufa kwa njaa katika mikoa ya Tigray na Amhara nchini Ethiopia katika miezi ya hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/4brjk
Ethiopia
Mvulana akijaribu kupanga magunia ya ngano wakati wa ugavi wa chakula cha msaada huko Amhara.Picha: Eduardo Soteras/AFP

Haya ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na taasisi ya taifa inayofuatilia utawala bora ambayo imekiri kadhia ya vifo vinavyotokana na njaa. 

Hapo awali, maafisa katika mikoa hiyo waliripoti vifo vilivyotokana na njaa katika wilaya za mikoa hiyo, lakini serikali ya shirikisho ya Ethiopia ilisisitiza kuwa ripoti hizo sio za kweli na taasisi hiyo ya taifa iliwatuma wataalamu katika mikoa iliyokumbwa na ukame na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika miezi 14 iliyopita.

Soma pia: Ethiopia yakanusha Tigray kunyemelewa na baa la njaa

Wataalamu hao waligundua kwamba jumla ya watu 351 walikufa kwa njaa katika mkoa wa Tigray ndani ya kipindi cha miezi sita iliyopita, na wengine 44 walikufa katika mkoa wa Amhara.

Kulingana na taarifa ya ndani iliyopatika na shirika la habari la Associated Press, ni sehemu ndogo tu ya watu wenye uhitaji huko Tigray wanaopokea misaada ya chakula, zaidi ya mwezi mmoja baada ya mashirika ya misaada kuanza tena kusambaza nafaka, baada ya kusimamishwa kwa muda kutokana na madai ya wizi.

Kwa mujibu wa asasi ya utoaji wa misaada ya chakula katika mkoa wa Tigray ya Food Cluster, ni asilimia 14 tu ya watu milioni 3.2 waliolengwa kupatiwa chakula kutoka kwa mashirika ya kibinaadam ya Tigray, waliopokea chakula kufikia Januari 21.

Juhudi za ziada zinahitajika

Ethiopia
Raia wanaoteseka kwa njaa, Tigray EthiopiaPicha: Million Hailesilassie/DW

Aidha taarifa hiyo ya ndani inahimiza vikundi vya kibinadamu kuzidisha opereshen zao, na kuonya kwamba kushindwa kuchukua hatua za haraka kunaweza kusababisha uhaba mkubwa wa chakula na utapiamlo na uwezekano wa kupoteza watoto na wanawake walio katika mazingira magumu zaidi katika mkoa huo.

Soma pia: Mamilioni ya watu wahitaji msaada wa chakula Tigray

Umoja wa Mataifa na Marekani zilisitisha msaada wa chakula kwa Tigray katikati ya Machi mwaka uliopita baada ya kugundua mpango "wa kiasi kikubwa" wa kuiba nafaka ya misaada ya kibinadamu. Maafisa wa Marekani wanaamini kuwa wizi huo unaweza kuwa wa kiwango kikubwa zaidi kuwahi kutokea na wafadhili wakiwalaumu maafisa wa serikali ya Ethiopia na jeshi kwa ulaghai.

Mnamo Disemba Umoja wa Mataifa na Marekani hatimaye waliondoa usitishwaji huo baada ya kufanya mageuzi ili kukabiliana na wizi, lakini mamlaka ya Tigray inasema chakula hakiwafikii wanaohitaji.

Licha ya mageuzi hayo wafanyakazi wawili wa misaada wamedai kwamba mfumo mpya uliowekwa, ambao unajumuisha kuweka vifuatiliaji vya GPS kwenye malori ya chakula na kuweka misimbo kwenye kadi za mgao zimetatizwa na changamoto za kiufundi huku mashirika ya misaada pia yakihangaika kutokana na ukosefu wa fedha.

 

//AP