Watu 4 wakamatwa Uganda kwa kumuua sokwe wa milimani
12 Juni 2020Sokwe huyo kwa jina Rafiki alikuwa kama kiongozi wa kundi la masokwe maalum 17, ambao ndio aina ya kwanza kuhamishiwa na kuishi nchini humo.
Sokwe huyo aliripotiwa kutoweka mnamo Juni 1, na mzoga wake ukapatikana siku ya pili ukiwa na majeraha tumboni.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la huduma kwa wanyama porini nchini Uganda, washukiwa wamedai walikuwa wakiwinda walipokutana na sokwe Rafiki pamoja na sokwe wengine. Kisha Rafiki akajaribu kuwashambulia, na katika hatua ya kujilinda, mwindaji mmoja akamchoma mkuki.
Maafisa hao wamesema mshukiwa mmoja amepatikana na ala za uwindaji zilizotumika ikiwemo mikuki.
Washukiwa hao wanne wanashikiliwa katika kituo cha polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Hatari ya sokwe hao kuangamia duniani
Uganda ina zaidi ya sokwe 500 wa milimani. Hiyo ikiwa zaidi ya nusu ya jumla ya sokwe hao 1,000 ambao wamesalia ulimwenguni.
Wanyama hao ambao wanakabiliwa na kitisho cha kutoweka duniani wamehifadhiwa kwenye mbuga ya kitaifa yenye ulinzi mkali ya Bwindi na Mghahinga. Wengine pia wanapatikana katika mbuga ya wanyama ya Virunga katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na mbuga ya kitaifa ya Volkano nchini Rwanda.
Sokwe wa milimani huletea nchi hizo mapato mengi ya fedha za kigeni kutokana na watalii wanaofika kuwatazama.