1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 27 wauawa wakimkumbuka kiongozi wa Kishia Kabul

6 Machi 2020

Watu waliojihami kwa silaha wamewaua raia 27 na kuwajeruhi wengine takriban 55 katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul Ijumaa wakati wa shughuli ya kumkumbuka kiongozi wa madhehebu ya wachache ya Shia, maafisa wamesema.

https://p.dw.com/p/3Yz52
Afghanistan Kabul Polizei erscheint nach Schießerei
Picha: picture-alliance/AP/R. Gul

Msemaji wa wizara ya afya Wahidullah Mayar amesema majeruhi wamepelekwa hospitalini mjini Kabul,  huku msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Nasrat Rahimi akisema kwa ujumla wahanga wote ni raia. Msemaji wa wizara ya afya hata hivyo amesema idadi ya vifo inaweza kuongezeka.

Duru kutoka jumuiya ya kujihami ya NATO zimesema kwamba idadi ya vifo ilikuwa juu zaidi ya watu 30, huku 42 wakiwa wamejeruhiwa na 20 miongoni mwao walikuwa na hali mbaya.

Viongozi kadhaa mashuhuri wa kisiasa waliohudhuria walinusurika, ikiwa ni pamoja na Abdullah Abdullah, mtendaji mkuu wa serikali ya muungano tangu mwaka 2014, na aliegombea uchaguzi wa rais mwaka jana.

Rais Ashraf Ghani amesema amezungumza kwa simu na mpinzani wake huyo, anayepinga tangazo la tume ya taifa ya uchaguzi lililotolewa mwezi uliopita lililomtangaza Ghani kama mshindi wa uchaguzi wa urais.

Ghani ameandika kwenye ukurasa wa twitter kwamba shambulizi hilo lilikuwa ni "uhalifu dhidi ya ubinaadamu na dhidi ya umoja wa kitaifa nchini Afghanistan".

Afghanistan Kabul | Anschlag auf schiitische Gedenkfeier
Mwanajeshi wa vikosi vya usalama vya Afghanistan,wakiwa kwenye eneo lililoshambuliwaPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Gul

Vikosi vya usalama vya Afghanistan bado vilikuwa vikijaribu kupambana na watu hao wenye silaha katika jengo ambalo halijakamilika ujenzi wake, amesema Rahimi. Idadi kubwa ya wanajeshi wamelizingira eneo hilo.

Taliban yakana kuhusika

Kundi la wanamgambo la Taliban limekana kuhusika na shambulizi hilo na wakati hakuna aliyekiri kuhusika, tawi la kundi la Dola la Kiislamu nchini humo limetangaza vita dhidi ya jamii ya Washia wachache. Wengi wa watu waliohudhuria shughuli hiyo walikuwa ni Washia.

Shambulizi hilo limefanywa siku kadhaa baada ya Marekani,Taliban wasaini makubaliano ya kihistoria mjini DohaMarekani na Taliban kusaini makubaliano ya amani, yanayotoa masharti kwa Marekani kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo, huku Taliban ikikabiliwa na jukumu la kupambana na ugaidi na kundi la IS.

Shughuli hiyo ya leo ilifanywa katika eneo linalokaliwa kwa kiasi kikubwa na watu wa madhehebu ya Shia karibu na mji mkuu, Kabul.

Pakistan Bombenanschlag in Hazara mit 89 Toten
Baadhi ya watu wa kabila ya Hazaraz wakiangalia masalia baada ya shambulizi la bomu mwaka 2013.Picha: Getty Images/AFP/B. Khan

Ni sherehe za kuadhimisha miaka 25 tangu kifo cha kiongozi wa kabila ya Hazaras ambao kwa kiasi kikubwa ni Waislamu wa Shia. Aliuawa mwaka 1995 na Taliban, wakati walipokuwa wakikaribia kudhibiti mji mkuu Kabul, ambao ulikuwa umeharibiwa na vita vibaya baina ya makundi ya mujahedeen, ambayo ni pamoja na Mazari.

Marekani yalaani

Jamaa za wahanga wa shambulizi hilo wamekusanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ambayo haiko mbali na eneo kulikotokea shambulizi, wengi wakimwagikwa na machozi wakati wakisubiri kuitambua miili ya wapendwa wao.

Balozi mdogo wa Marekani nchini humo Ross Wilson ameandikwa kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba "tunalaani vikali shambulizi hilo la leo... Tunasimama na Afghanistan kwa ajili ya amani." Shambulizi hilo lilikuwa ni moja ya mashambulizi makubwa dhidi ya raia nchini Afghanistan kwa mwaka mmoja sasa.

"Shambulizi linalotisha limetokea Kabul leo.. inasikitisha na haikubaliki. Tumechoshwa na vita na mapigano," amesema Shahrzad Akbar, mkuu wa tume ya huru ya haki za binaadamu ya Afghanistan.

Vyanzo: rtre, afp