1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 240 wauawa Ethiopia

8 Julai 2020

Kiasi watu 240 wameripotiwa kuuawa nchini Ethiopia, kufuatia kifo cha mwanamuziki maarufu Hachalu Hundessa na kusababisha machafuko kote nchini humo. Hachalu alipigwa risasi mjini Addis Ababa

https://p.dw.com/p/3eyJ8
USA| Protest nach Tod von äthiopischem Sänger und Aktivisten Hachalu Hundessa
Picha: Getty Images/S. Maturen

Inaelezwa kwamba kumekuwepo na taarifa kidogo mno kuhusiana na mazingira ya kifo cha mwanamuziki huyo. Mkuu wa tume ya kipolisi ya mkoa wa Oromia Mustefa Tadir, amesema kiasi watu 229 ikiwa ni pamoja na wanajeshi walikufa katika machafuko katika mkoa huo, wakati kulipoibuka maandamano yaliyogubikwa na machafuko. Tadiri alikuwa akizungumza na shirika la habari lenye mahusiano na serikali la Walta Info.

Kulingana na polisi, raia wanane na polisi wawili waliuawa katika mji mkuu Addis Ababa tangu maandamano hayo yalipoanza, na watu 3,500 walikamatwa wakihusishwa na machafuko hayo. Hali katika mji mkuu wa Oromia hadi hii leo ilikuwa tete na iliyogubikwa na ukimya, huku huduma za intaneti zikiwa zimekatwa na serikali kwa siku tisa sasa, ili kupunguza kasi ya watu kuhimizana kuandamana kupitia mitandao ya kijamii.

Meya wa jiji la Shashemene Temam Hussein ameliambia shirika la habari la DW kwamba kumetokea visa vingi vya nyumba na majengo kuchomwa moto na nusu yake hayafai tena kwa makazi, lakini pia shule na maduka vilichomwa.

Äthiopien Hachalu Hundessa, ermordeter Künstler
Mwanamuziki aliyeuawa nchini Ethiopia Hachalu Hundesa, na kifo chake kimesababisha maandamano makubwaPicha: Leisa Amanuel

Alisema "Kiasi majengo marefu 20 yamechomwa moto. Kiasi makazi 201 ya familia pia yamechomwa. Majengo marefu yasiyopungua 15 yameharibiwa. Nusu ya majengo hayo hayakaliki tena. Magari yasiyopungua 78 pia yamechomwa. Maduka 28 yalichomwa moto, shule mbili pia zilichomwa na tukio hilo lilikuwa kubwa na baya sana."

Aidha mmoja wa waathirika wa machafuko hayo aliiambia DW kwamba hata raia ambao hawakuonyesha misimamo yao ya kisiasa walipigwa na kuuawa kikatili. "Wakulima watatu wasiokuwa na msimamo wowote wa kisiasa waliuawa kikatili. Walishambuliwa vibaya sana kwa visu vikali na mapanga. Mauaji hayo yalifanyika kwa siku tatu." alisema mwathirika huyo.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema mauaji ya Hachalu pamoja na maandamano ya baada ya kifo hicho yalikuwa sehemu ya mpango wa kuzusha machafuko nchini humo.

Hachalu alizikwa Julai 2 nyumbani kwake Ambo, katikati ya mkoa wa Oromia huku kukiwa na ulinzi mkali. Wengi waliuona muziki wake kuwa uliolezea haki za watu wa kabila ya Oromo, ambao kwa muda mrefu walijihisi kutengwa na serikali.

Soma Zaidi: Maoni: Kifo cha mwanamuziki maarufu nchini Ethiopia

Mashirika: DPAE/AFPE.