Watu 14 wauwawa katika shambulio kusini magharibi ya Kongo
13 Agosti 2023Msemaji wa serikali ya mkoa wa Kwango Adelard Nkisi amesema kundi la wanamgambo liliwashambulia raia kwa risasi na mapanga. Wanamgambo hao pia walichoma moto nyumba kadhaa katika kijiji hicho kilicho umbali wa kilometa 370 kusini magharibi mwa mji mkuu, Kinshasa.
Nkisi amesema kuwa raia wengine ambao idadi yao haijafahamika walifungwa na kutekwa na wanamgambo hao ambao baadaye walikimbilia vichakani.
Kiongozi wa kidini kwenye kijiji hicho aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema shambulio hilo lilitokana na hatua ya hivi karibuni ya kukamatwa kwa wanamgambo ambao walituma timu yao kuwaokoa wenzao. Kiongozi mwingine wa asasi ya kijamii katika mkoa huo, Symphorien Kwengo amelinyooshea kidole cha lawama kundi la wanamgambo wa Mobondo kwa kuhusika na shambulio hilo.