1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 12 waelezwa kuuwawa kwa mashambulizi ya Israel Gaza

29 Juni 2024

Maafisa wa afya wa Palestina wamesema watu 12 wameuwawa katika mashambulizi mapya katika Ukanda wa Gaza, huku jeshi la Israel likisema mashambulizi yake yamelenga eneo la Shejaiya mashariki mwa mji huo.

https://p.dw.com/p/4hfPj
Mzozo wa Israel na Palestina - Rafah
Mzozo kati ya Israel na Palestina, Moshi waongezeka baada ya mashambulizi ya anga ya Israel katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Maafisa wa afya wa Palestina wamesema watu 12 wameuwawa katika mashambulizi mapya katika Ukanda wa Gaza, huku jeshi la Israel likisema mashambulizi yake yamelenga eneo la Shejaiya mashariki mwa mji huo, yakiwemo maeneo mengine ya wanamgambo wanaodaiwa kuwa na nia ya kuwashambulia wanajeshi wa Israel.

Jeshi hilo pia limesema limefanya mashambulizi ya ardhini dhidi ya watu waliokuwa wamejihami kwa silaha waliokuwa katika mahandaki. Pia imeripoti kukamata silaha kadhaa katika operesheni yao.

Maafisa wa afya wamesema watoto nimiongoni mwa waliouwawa katika mashambulizi hayo. Shirika la habari la Palestina la WAFA limesema nyumba za wakaazi ni miongoni mwa majengo yaliyolengwa. Siku ya Alhamisi Israel iliwataka wakaazi wa eneo hilo kuondoka kabla ya kushambulia.

Wizara ya afya inayoongozwa na Hamas imesema tangu mapigano yalipoanza kati ya Israel na wanamgambo hao Oktoba 7, watu zaidi ya 37,000 wameuwawa huku watu zaidi ya 85,000 wakijeruhiwa katika mapigano hayo yaliyodumu kwa miezi 9 sasa.