1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 10 wauawa katika mashambulizi ya anga Tigray

Sylvia Mwehozi
15 Septemba 2022

Watu 10 wameuawa katika siku ya pili ya mashambulizi ya anga kwenye mkoa wa Tigray nchini Ethiopia huku serikali ya nchi hiyo ikielezea utayari wa kushiriki mchakato wa amani kufuatia wito wa jumuiya ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/4Gsvn
 Äthiopien Luftangriff  in Mekele, Tigray
Picha: Million Haileselassie/DW

Mashambulizi pacha ya ndege zisizo na rubani yamepiga katika kitongoji cha mji mkuu wa Tigray wa Mekele jana na kuwaua watu 10 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, kulingana na maafisa wawili wa hospitali kubwa mjini humo. Mashambulizi hayo ya anga yametokea baada ya mamlaka za mji wa Tigray kutangaza siku ya Jumapili kwambawako tayari kwa mazungumzo yanayoongozwa na Umoja wa Afrika kwa ajili ya kumaliza vita vya karibu miaka miwili huko kaskazini mwa Ethiopia.

Msemaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF, Kindeya Gebrehiwot, alisema kupitia ukurasa wa Twitter kwamba "utawala wa Addis unaendelea kukaidi uwezekano wowote wa suluhisho la amani kwa njia ya mashambulizi ya nguvu na mashambulizi ya anga."

Mashambulizi hayo ya Jumatano yanafuatia shambulio jingine la ndege isiyo na rubani lililotokea siku ya Jumanne katika Chuo Kikuu cha Mekelle, ambako mamlaka za Tigray zilisema lilisababisha majeraha na uharibifu wa mali.Vikosi vya angani vya Ethiopia vyashambulia Mekele, Tigray

Wakati mashambulizi hayo yakiripotiwa, serikali ya Ethiopia kupitia wizara ya mambo ya nje ilisema hapo jana kwamba "inajitolea" katika mchakato wa mazungumzo ya amani yanayoratibiwa na Umoja wa Afrika ili kuutafutia ufumbuzi mzozo huo. Tangazo hilo ni la kwanza kutolewa na serikali tangu mamlaka za Tigray kuashiria utayari wake katika kusitisha mapigano na kushiriki mchakato wa amani.

Luftangriff trifft Mekelle, Region Tigray
Wahudumu wa afya wakiwa wamebeba mwili wa mtu aliyejeruhiwaPicha: AP/picture alliance

Taarifa iliyochaishwa katika ukurasa wa Facebook imemnukuu naibu waziri mkuu na ambaye ni waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Demeke Mekonnen akisema kwamba "serikali itaunga mkono juhudi za kumaliza mgogoro huo kwa amani".  Chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF katika siku za nyuma kilipinga mjumbe wa Umoja wa Afrika katika pembe ya Afrika Olusegun Obasanjo kuwa mpatanishi wa mzozo huo, kikiitaka Kenya kuwa mpatanishi wa mazungumzo yoyote.Kumi wauwawa katika shambulio Ethiopia

Jumuiya ya kimataifa imezitolea mwito pande zote kutumia wakati huu kujaribu kukomesha vita ambavyo vimewaua idadi ya raia ambao haijatajwa na kuchochea mgogoro mkubwa wa kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Mkuu wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat na Jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika IGAD wamekaribisha utayari wa pande zote mbili kushiriki mchakato wa amani.

Umoja wa Ulaya kwa upande wake umeelezea wasiwasi juu ya mashambulizi ya hivi karibuni ya anga ukisema yanahatarisha "matumaini ya amani".