1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watawala wapya Syria wateua waziri wao wa mambo ya nje

21 Desemba 2024

Kundi lililoongoza mapinduzi dhidi ya Bashar al-Assad nchini Syria limemteua Assad al-Shibani kuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya mpito. Al-Shibani alikuwa miongoni mwa maafisa wa serikali ya uokoaji ya Idlib.

https://p.dw.com/p/4oT5B
Syria | Kiongozi mpya Ahmed Al-Sharaa
Kiongozi mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa.Picha: SANA/AP/dpa/picture alliance

"Kamandi kuu inatangaza uteuzi wa Bw. Assaad Hassan al-Shibani kuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali mpya ya Syria," ilissema taarifa. 

"Alijiunga na mapinduzi ya Syria mwaka 2011... na alishiriki katika kuanzisha Serikali ya Uokoaji," yalisema maandishi yaliyochapishwa kwenye Telegram. 

Serikali ya Uokoaji, ambayo ina wizara, idara, mamlaka za kisheria na usalama, ilianzishwa mwaka 2017 kusaidia watu waliokatiwa huduma za serikali. 

Wengi wa mawaziri wapya nchini Syria wanatoka kwenye kile kinachoitwa "Serikali ya Uokoaji". 

Shibani alizaliwa mwaka 1987 katika jimbo la Hasakeh kaskazini-mashariki mwa Syria, na alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Damascus katika fasihi ya Kiingereza kabla ya kuchukua shahada ya uzamili katika sayansi ya siasa na mahusiano ya kimataifa. 

Assad akimbia nchi, waasi waukamata Damascus

Pia akijulikana kwa jina la Zaid al-Attar, alikutana na wajumbe kutoka Ufaransa na Ujerumani waliotembelea Damascus wiki hii kufungua mawasiliano na mamlaka mpya. 

Soma pia: Utawala mpya wa Syria wataka kuchangia "amani ya kikanda" na kupinga migawanyiko

Ijumaa, baada ya mkutano kati ya kiongozi mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa na ujumbe wa Marekani, mamlaka mpya zilisema zinataka kuchangia "amani ya kanda" na "kujenga ushirikiano wa kimkakati wa kipaumbele na nchi za kanda". 

Taarifa ya Ijumaa pia ilisema "watu wa Syria wamesimama kwa usawa na nchi zote na vyama katika kanda na kwamba Syria inakataa mgawanyiko wowote."

Qatar yafungua tena ubalozi wake Damascus

Qatar ilifungua tena ubalozi wake mjini Damascus siku ya Jumamosi, miaka 13 baada ya kufungwa mwanzoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, wakati serikali za kigeni zikijaribu kuanzisha uhusiano na watawala wapya wa nchi hiyo. 

Mwandishi wa AFP aliiona bendera ya Qatar ikipandishwa juu ya ubalozi huo, na kuifanya Qatar kuwa taifa la pili, baada ya Uturuki, kufungua rasmi ubalozi wake tangu waasi walioongozwa na kundi la Hayat Tahiri al-Sham, HTS, kumwondoa rais Bashar al-Assad madarakani mapema mwezi huu. 

Tofauti na serikali nyingine kadhaa za Kiarabu, Qatar — ambayo iliunga mkono makundi ya upinzani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria — haikujaribu kufanya maridhiano na Assad kabla ya kuondolewa kwake madarakani. 

Mapema Jumamosi, wafanyakazi walikuwa wakisafisha barabara, kusafisha eneo hilo na kuondoa maandishi ya graffiti kutoka kwenye kuta za jengo hilo. Mmoja wa wafanyakazi aliweka bendera ya Qatar kwenye msingi wa nguzo ya bendera. 

Soma pia: HTS kujivunja na kujiunga na jeshi la Syria

Doha ilituma ujumbe wa kidiplomasia kwenda Damascus siku chache zilizopita ili kukutana na serikali ya mpito. Ujumbe huo ulionyesha "dhamiri kamili ya Doha kuunga mkono watu wa Syria", mwanadiplomasia wa Qatar aliiambia AFP. 

Jumanne, Umoja wa Ulaya ulisema uko tayari kufungua tena ujumbe wake wa kidiplomasia mjini Damascus, huku Uingereza, Ufaransa na Marekani zote zikituma ujumbe kwenda mji mkuu wa Syria tangu kuondolewa kwa Assad madarakani. 

Syria Damaskus | Ubalozi wa Uturuki
Qatar imekuwa nchi ya pili kufungua tena ubalozi wake mjini Damascus baada ya Uturuki kuchukuwa hatua hiyo mara tu baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad.Picha: Amr Abdallah Dalsh/REUTERS

Bendera ya Ufaransa ilipandishwa juu ya ubalozi wa Paris mjini Damascus Jumanne, ingawa mjumbe maalum wa nchi hiyo kwa Syria alisema ubalozi huo utabaki kufungwa "hadi vigezo vya usalama vitakapokidhiwa". 

Wakati huo huo, Marekani siku ya Ijumaa ilifuta zawadi ya dola milioni 10 ambayo ilikuwa imetangaza miaka iliyopita kwa Ahmed al-Sharaa, kiongozi mpya wa Syria na mkuu wa kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham ambalo liliongoza mapinduzi dhidi ya Assad. 

Wanadiplomasia wa Marekani wafanya "mazungumzo chanya" na watawala wapya

Wajumbe waandamizi wa Marekani walifanya mazungumzo mazuri na Ahmed al-Sharaa, mtawala mpya wa muda wa Syria, siku ya Ijumaa kuhusu mchakato wa mpito wa kisiasa nchini humo.

Soma pia: Iran yazishutumu Israel, Marekani kwa anguko la Assad

Barbara Leaf, afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na Mashariki ya Kati, alikutana na al-Sharaa, kiongozi wa kundi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS), ambalo liliongoza mashambulizi ya waasi yaliyomwondoa Bashar al-Assad madarakani mapema Desemba. 

Bahrain Manama 2024 | Mwanadiplomasia wa Marekani Barbara Leaf
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani anaeshughulikia kanda ya mashariki ya karibu Barbra Leaf aliongoza ujumbe wa kwanza wa Marekani nchini Syria na kuzungumza na kiongozi wa mpito Ahmed al-Sharaa.Picha: Mazen Mahdi/AFP

Mazungumzo hayo yalihusisha pia wajumbe Roger Carstens, mjumbe maalum wa Marekani anaeshughulikia mateka, na Daniel Rubinstein, mjumbe maalum wa Marekani kwa Syria.

Leaf alieleza kuwa mazungumzo hayo yalijikita katika umuhimu wa kuhakikisha kuwa makundi ya kigaidi hayaleti tishio ndani ya Syria wala nje ya mipaka yake.

Kufuatia mazungumzo hayo, Marekani iliamua kuondoa zawadi ya dola milioni 10 iliyokuwa imetangazwa kwa al-Sharaa, ambaye zamani alijulikana kama Mohammed al-Joulani. 

Ziara hiyo ilikuwa ya kwanza kufanywa na wanadiplomasia wa Marekani tangu kuondolewa kwa al-Assad, ambaye amekimbilia Moscow.

Huku Marekani ikiwa imewahi kuwasiliana na HTS hapo awali, inakabiliwa na changamoto ya jinsi ya kushughulika na kundi hilo, ambalo bado linachukuliwa kama shirika la kigaidi.

Hata hivyo, hili halikuwazuia wanadiplomasia wake kukutana na wawakilishi wa HTS kwa mazungumzo. 

Wajumbe hao wa Marekani pia walikutana na wanachama wa mashirika ya kiraia, wafanyakazi wa kiutu, na wengine kujadili maono yao kuhusu mustakabali wa Syria na jinsi Marekani inavoyweza kuwasaidia.

Soma pia: Mohammed al-Bashir kiongozi wa mpito Syria

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisisitiza dhamira yake ya kuunga mkono mchakato wa mpito wa kisiasa unaoongozwa na Wasyria wenyewe, na ambao ni shirikishi. 

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vilianza mwaka 2011 kufuatia maandamano ya kupigania demokrasia dhidi ya utawala wa al-Assad.

Mwaka uliofuata, Marekani ilisitisha mahusiano ya kidiplomasia na Syria, lakini inaonekana sasa inatafuta njia za kuanzisha tena ushirikiano kupitia mchakato wa mpito unaoongozwa na serikali ya mpito ya HTS.

Vyanzo: afpe,rtre,dpa