1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watawala wa zamani waongoza mbio za urais Madagascar

Oumilkheir Hamidou
5 Novemba 2018

Raia wa Madagascar watapiga kura Jumatano kuchagua rais mpya, ambapo marais watatu wa zamani wanaongoza kinyanganyiro cha kuongoza taifa hilo la kisiwa lililotikiswa na mmgogoro mwanzoni mwa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/37hLy
Madagaskar Wahlen Plakate in Antananarivo
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Wagombea 36 wanashindania kiti cha Urais ikiwa ni duru ya kwanza katika uchaguzi itakaoitishwa Jumatano kisiwani Madagascar-lakini kinyang'anyiro kitakuwa kati ya wagombea watatu wanaopewa nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi na wote ni marais wa zamani wa kisiwa hicho cha bahari ya Hindi.

Marc Ravalomanana, mwenye umri wa miakam 68, bado hajakubali kumeza machungu ya kutimuliwa kwake madarakani mwaka 2009 na amepania kulipiza kisasi kupitia vituo vya kupiga kura. Muuza maziwa huyo wa zamani amejipatia umaarufu katika sekta ya biashara na kubuni kampuni kubwa la maziwa ya kuganda au mtindi kwa jina Tiko.

Marc Ravalomanana anaejinata amechapa kazi hadi kufikia alipofikia, ni miongoni mwa matajiri wakubwa wa Madagascar, kwa mujibu wa jarida la Marekani Forbes, ameingia kwa kishindo katika jukwaa la kisiasa aliposhinda uchaguzi wa meya wa mji mkuu Antananarivo mwaka 1999.

Madagaskar Wahlen Kandidat Ravalomanana
Rais wa zamani Marc Ravalomanana akiwasalimu wafuasi wake wakati wa kampeni katika uwanja wa mpira wa Mahasina mjini Antananarivo, Agosti 25, 2018.Picha: Getty Images/AFP/Rijasolo

Miaka miwili baadae akamshinda katika uchaguzi wa rais uliogubikwa na machafuko, Didier Ratsiraka aliyekuwa akigombea mhula mwengine madarakani. Mwaka 2006 akachaguliwa moja kwa moja katika duru ya akwanza baada ya kufanikiwa kufutiwa deni la Madagascar. Lakini katika wakati ambapo wafuasi wake walikuwa wanasifu ufanisi wake wapoinzani wake walikosoa utawala wake wa mkono wa chuma.

February 7 mwaka 2009 kikosi cha ulinzi wa rais kikatumia nguvu kukandamiza maaandamano ya amani kuelekea kasri la rais, maandamano yaliyoitishwa na wafuasi wa meya kijana wa Antananarivo Andry Rajaoelina.

Akitengwa na jeshi, Marc Ravalomanana akaukabidhi madaraka uongozi wa kijeshi ambapo kwa upande wao wakamkabidhi hatamu za uongozi hasimu yake Andry Rajoelina. Alilazimika kukimbilia uhamishoni hadi mwaka 2014.

Akihojiwa Jumapili iliyopita na shirika la habari la ufarana AFP, jibu lake litakuwa la aina gani pindi Rajoelina akishinda uchaguzi wa rais mwaka huu,Marc Ravalomanana alisema "nitakubali kushindwa lakini kwa sharti hakujakua na visa vya rushwa wala udanganyifu."

Madagaskar Wahlen Kandidat Rajoelina
Rais wa zamani Andry Rajoelina akiwasalimia wafuasi wake katika uwanja wa michezo wa Mahamasina, Agosti 1, 2018.Picha: Getty Images/AFP/Rijasolo

Andry Rajoelina: Sikuwa na uzoefu wa kuendesha serikali

"Akipewa jina la utani la TJV" kutokana na juhudi zake za kasi, Andry Rajoelina, mwenye umri wa miaka 44 hivi sasa ameingia katika jukwaa la kisiasa tangu mwaka 2007. Akijipatia umashuhuri kutokana na maandalizi yake ya burudani katika mji mkuu Antananarivo, kiongozi huyo kijana wa shirika la uchapishaji alizusha maajabu alipochaguliwa kuwa meya wa Antananarivo mwaka huo huo wa 2007.

Alijitokeza kuwa mshika bendera wa wapinzani wa Ravalomanana kutokana na werevu wake katika kutumia vyombo vya mawasiliano na kupitia kituo chake cha televisheni Viva.Wafuasai wake hawakuogopa kukinzana na serikali na kuitisha maandamano majiani akijivunia uungaji mkono wa kichini chini wa jeshi.

Lakini mpaka leo Adry Rajoelina anakanusha anasema hajaingia madarakani kupitia mapinduzi."Yalikuwa maandamano ya umma. Nasikitika tu kwamba sikuwa na maarifa ya kutosha kuongoza serikali," alisema alipohojiwa na shirika la habari la AFP.

Madagaskar Präsident Hery Martial Rakotoarimanana Rajaonarimampianina
Mgombea mwingine wa urais, rais aliamaliza muda wake Hery Martial Rajaonarimampianina.Picha: Reuters

Mgombea wa tatu ni rais anaemaliza mhula wake Hery Rajaonarimpianina mwenye umri wa miaka 60. Yeye pekee ndie mkimya miongoni mwa wagombea hao watatu wanaopewa nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi.

Alipoingia madarakani mwaka 2013, mtaalam huyo wa masuala ya kiuchumi na mtunzi wa mashairi alipanga kuanzisha ukurasa mpya baada yaa miaka kadhaa ya mizozo kisiwani Madagascar.

Lakini mhula wake 2014 hadi 2018 haujakwepa matumizi ya nguvu. Amenusurika katika majaribio mawili ya kumng'owa madarakani na machafuko ya umma yaliyopelekea watu wawili kuuwawa.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman