1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watanzania 206 warejesha nyumbani kutoka Sudan

George Njogopa27 Aprili 2023

Raia wa Tanzania wapatao 206 waliokuwa nchini Sudan wamerejeshwa leo na serikali kufuatia mapigano yanayoendelea nchini humo. Raia hao ni wanafunzi, wafanyakazi wa ubalozi pamoja na raia wa kawaida.

https://p.dw.com/p/4QdHV
Air Tanzania
Picha: flickr/stevesaviation

Watanzania hao ambao asilimia kubwa ni wanafunzi wanaosoma nchini humo waliwasili leo kwa kutumia ndege ya shirika la ndege la Tanzania ATCL iliyotumwa na serikali kama hatua ya kuwanusuru kufuatia mapigano yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo tangu wiki iliyopita.

Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Julius Nyerere, raia hao wakiwa wameambatana na balozi wa Tanzania nchini humo walilakiwa na waziri wa mambo ya nje wa Tanzania pamoja na ndugu na jamaa zao.

Soma pia: Tanzania yalaani mapigano yanayoendelea Sudan

Safari yao ya kujinasua kutoka Khartoum hadi Dar es salaam inatajwa kuwa ya milima na mabonde, wakisafiri kwa miguu na basi kutoka mji mkuu wa Sudan hadi mji ulioko jirani na Ethiopia. Waziri wa mambo ya nje, Stegormena Tax amesema, imekuwa jambo la heri kwa watanzania hao kurejea nyumbani wakiwa salama.

Watanzania hao ni sehemu ya raia wengi wa kigeni wanaosafirishwa na mataifa yao kurejea nyumbani kwa hofu ya usalama wa maisha yao kutokana na mapigano yanayoendelea yakihusisha kikosi cha jeshi la Sudan na kikosi cha RFS.

Akizungumza mara baada ya kuwasili nchini, mmoja wa wanafunzi hao hakuwa na mengi ya kusema mbali ya kushuhudia adha waliyoipita huku akitafakari falsafa ya amani na mshikamano.

Balozi wa Tanzania nchini Sudan Salima Kombo amesema upo uwezekano mkubwa kwa Watanzania wengine waliosalia nchini humo akimaanisha kuwa uwezekano huo unatokana na pengine kukosa taarifa za sehemu wanazoishi na shughuli wazifanyazo.

Serikali haijasema lolote iwapo itatuma tena ndege nyingine iwapo kutajitokeza idadi kubwa ya Watanzania wanaoendelea kukwama nchini humo kutokana na mapigano yanayoendelea.

Licha ya Tanzania kutopakana moja kwa moja na taifa hilo la Sudan lakini duru za habari zinaonyesha kuwepo kwa muingiliano mkubwa wa raia wa pande hizo mbili kutokana na  mahitaji ya kibiashara na fursa za elimu.