1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataliani wapiga kura

Sekione Kitojo
4 Machi 2018

Wataliani wanapiga kura Jumapili(04.03.2018)katika uchaguzi unaoweza kuleta mkwamo wa kisiasa baada ya kampeni ambayo imegubikwa na hasira kuhusiana na kudorora kwa uchumi, idadi kubwa ya wasio na kazi na uhamiaji.

https://p.dw.com/p/2teip
Italien Wahlen Stimmzettel
Picha: picture alliance/AP Photo/M. Bazzi/ANSA

Mashirika yanayofanya utafiti wa  maoni  ya wapiga  kura yanatabiri  kwamba waziri  mkuu  wa  zamani  Silvio Berlusconi  na  washirika  wake  wa  siasa kali  za  mrengo  wa  kulia  wataibuka  kuwa  kundi  kubwa  bungeni, lakini wakikosa  wingi  wa  kutosha.

Italien Wahlkampf Partito Democratico, Matteo Renzi
Waziri mkuu wa sasa wa Italia Matteo RenziPicha: picture-alliance/NurPhoto/G. Maricchiolo

Vuguvugu  la  kupinga  utawala  la  5-Star linaonekana  litakuwa  chama kikubwa pekee, kikipata  nguvu  kutokana  na  wapiga  kura  kutoridhishwa na rushwa  iliyoota  mizizi na  ongezeko  la  umasikini, wakati  chama  tawala  cha siasa za  wastani  za  mrengo  wa  kushoto cha  Democratic kinaonekana kikipata  nafasi  ya tatu.

"Kumekuwa  na msukumo kwa  upande  wa  vuguvugu  la 5-Star katika  siku za  mwisho za  kampeni, lakini  ni  vigumu  kuona chama  chochote ama muungano  wa  vyama  ukipata asilimia 40  zinazohitajika  kuunda  serikali," amesema Lorenzo Pregliasco, muasisi  mwenza wa shirika  la  utafiti  wa maoni  ya  wapiga  kura  la YouTrend.

Italien Silvio Berlusconi
Waziri mkuu wa zamani Silvio BerlusconiPicha: Reuters/M. Rossi

Madeni ya  taifa

Italia  ambayo  ina  madeni mpaka  shingoni ni uchumi  wa  tatu  katika mataifa  19 ya kanda  ya  sarafu  ya  euro  na  licha  ya  kwamba  wawekezaji wamekuwa  wenye matumaini  kabla  ya  uchaguzi  wa  leo, mkwamo  wa kisiasa  uliorefushwa unaweza  kufufua  kitisho cha kutokuwa  na  uthabiti wa masoko.

Italien Wahl 2018
Wafanyakazi wa kituo cha kupigia kura wakitayarisha karatasi za kuraPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Calanni

Vituo vya  kupigia  kura  vitafunguliwa  kuanzia  saa moja  asubuhi  leo hadi saa tano  usiku , ambapo matokeo  ya  awali yanatarajiwa  mara tu  baada  ya vituo  kufungwa. Uchaguzi  huo  unafanyika  chini  ya  sheria  mpya  ya uchaguzi  yenye  utata ambayo  ina  maana  matokeo  ya  mwisho huenda hayatakuwa  wazi  hadi Jumatatu.

EU Antonio Tajani
Rais wa bunge la Ulaya Antonio Tajani ambaye anawania wadhifa wa waziri mkuu wa ItaliaPicha: picture alliance/ZUMAPRESS/C. Mahjoub

Kampeni  zimeshuhudia kurejea  katika  mstari  wa  mbele  wa siasa Berlusconi  mwenye  umri  wa  miaka  81, ambaye  alilazimika  kuachia wadhifa  wa  waziri  mkuu  mwaka  2011  wakati  wa  mzozo  mkubwa  wa madeni  ya  ndani  na  aliondolewa  kutokana  na  mlolongo  wa  kashfa za ngono, mivutano ya  kisheria  pamoja  na  afya mbaya.

Hukumu  ya  mwaka  2013 kwa  udanganyifu  wa  kulipa  kodi  ulikuwa  na maana  hawezi  tena  kuwa  kiongozi  wa  umma na  amemuweka  mbele Antonio Tajani, Rais wa  bunge  la  Ulaya , kuwa  mgombea  wa  kiti  cha waziri  mkuu.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Caro Robi