Wataalamu: Mifumo ya Urusi iliiangusha ndege ya Azerbaijan
27 Desemba 2024Ndege ya Azerbaijan Airlines aina ya Embraer 190 ilikuwa ikisafiri kutoka mji mkuu wa Azerbaijan, Baku, kwenda Grozny, mji ulioko Kaskazini mwa Caucasus nchini Urusi, siku ya Jumatano ilipoelekezwa kwenye njia nyingine kwa sababu ambazo bado hazijafahamika na kuanguka wakati wa jaribio la kutua Aktau, Kazakhstan, baada ya kuruka mashariki kupitia Bahari ya Caspian.
Ajali hiyo ilitokea takriban kilomita 3 kutoka Aktau, ambapo picha za simu za mkononi zilizosambazwa mtandaoni ziliionyesha ikishuka kwa kasi kabla ya kuanguka na kulipuka kwa moto mkubwa. Picha nyingine zilionyesha sehemu ya nyuma ndege hiyo ikiwa imekatikia kwenye mabawa na ikiwa imelala juu chini kwenye nyasi.
Azerbaijan iliomboleza waathirika wa ajali hiyo Alhamisi kwa kushusha bendera nusu mlingoti kitaifa. Trafiki ilisimama saa sita mchana huku meli na treni zikilia king'ora kwa dakika ya ukimya kuwakumbuka waliofariki.
Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, alisema katika mkutano wa waandishi wa habari kuwa bado ni mapema kuhitimisha sababu za ajali hiyo lakini alieleza kuwa hali mbaya ya hewa ilisababisha ndege hiyo kubadili njia yake.
Soma pia: Takriban watu 28 waokolewa wakiwa hai katika ajali ya ndege
Mamlaka ya anga ya Urusi, Rosaviatsia, iliripoti kuwa taarifa za awali zinaonyesha kwamba rubani alielekea Aktau baada ya ndege kugongana na ndege nyingine, hali iliyosababisha dharura. Hata hivyo, mamlaka za Azerbaijan, Kazakhstan, na Urusi zimekuwa kimya kuhusu chanzo halisi cha ajali hiyo.
Mbunge aitaka Urusi kubeba lawama na kutoa fidia
Mbunge wa Azerbaijan, Rasim Musabekov, alidai kuwa ndege hiyo ilipigwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi wakati ikipita angani juu ya Grozny na akataka Urusi iombe msamaha rasmi na kulipa fidia kwa wahanga. Wataalamu wengine walieleza mashimo kwenye sehemu ya mkia wa ndege hiyo kuwa ishara ya kushambuliwa na kombora dogo la ardhini.
Shirika la Osprey Flight Solutions, ambalo linajishughulisha na usalama wa anga, alisema kwamba ndege hiyo huenda ilitunguliwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi, Pantsyr-S1, huku wataalamu wakiongeza kuwa picha za mkia wa ndege zinaonyesha uharibifu unaoendana na vipande vya kombora.
Tovuti ya Caliber ya Azerbaijan yenye uhusiano mzuri na serikali, ilidai kwamba ndege hiyo ilipigwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi huku ikihoji kwa nini mamlaka za Urusi hazikufunga uwanja wa ndege licha ya mashambulizi ya droni katika eneo hilo.
Soma pia: Ndege ya abiria ya Azerbaijan yaanguka
Kremlin kupitia msemaji wake, Dmitry Peskov, ilionya dhidi ya hitimisho la mapema na kusema kuwa ni muhimu kusubiri uchunguzi rasmi wa ajali hiyo. Aidha, spika wa bunge la Kazakhstan, Maulen Ashimbayev, alionya dhidi ya kutumia picha za mabaki ya ndege hiyo kama msingi wa madai.
Miongoni mwa waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni raia 42 wa Azerbaijan, 16 wa Urusi, 6 wa Kazakhstan, na 3 wa Kyrgyzstan. Wizara ya Dharura ya Urusi siku ya Alhamisi iliwahamisha manusura 9 wa Urusi kwenda Moscow kwa matibabu zaidi.