1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiIran

Washukiwa wakamatwa Iran kuhusiana na sumu katika shule

Daniel Gakuba
7 Machi 2023

Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Iran ametangaza mamlaka za nchi hiyo zimewakamata watu kadhaa wanaoshukiwa kuhusika na wimbi la kuwalisha sumu wasichana ambalo limesababisha mtafaruku wa miezi kadhaa nchini humo.

https://p.dw.com/p/4OMZz
Iran Protest
Picha: Diego Radames/SOPA Images via ZUMA Press Wire/ZUMAPRESS/picture alliance

Afisa huyo, Majid Mirahmadi, amesema uchunguzi wa kiintelijensia umewezesha kukamatwa kwa watu katika mikoa mitano, na vyombo vinavyohusika vinaendesha uchunguzi wa kina.

Tatizo hilo limeshuhudiwa katika mikoa 25 kati ya 31 iliyopo Iran, ambapo wanafunzi zaidi ya 5,000 katika shule 230 wameripoti matatizo ya kushindwa kupumua na kusikia kizunguzungu, na baadhi walipelekwa hospitalini.

Hali hii imewakasirisha wazazi ambao wamekuwa wakiishinikiza serikali kuchukua hatua haraka.

Harufu isiyo ya kawaida ilisikika katika shule husika, na mmoja wa wabunge wanaofuatilia suala hilo amesema wanafanya vipimo kadhaa kubainisha aina ya sumu iliyotumiwa.