Wanamgambo washambulia shule Mandera
23 Novemba 2016Bado haijabainika iwapo washambuliaji hao walikuwa wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa al-Qaida.
Washambuliaji hao waliingia katika darasa ambako wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari walikuwa wanafanya mtihani na kuanza kurusha risasi.
Polisi waliokuwa wanalinda sehemu hiyo walilazimika kujibizana kwa risasi na kundi hilo kabla wapiganaji hao kutoroka.
Kamishna wa Kaunti ya Wajir, Mohamud Saleh, ameeleza kuwa polisi sita walikuwa wanalinda eneo hilo wakati mitihani ilipokuwa inaendelea.
Kundi la al-Shabaab limehusika na mashambulizi ya mara kwa mara kaskazini mwa Kenya ikiwa ni pamoja na yale ya kwenye Chuo Kikuu cha Garissa mwezi Aprili 2015, ambapo watu 148 waliuwawa.
Eneo ambalo mashambulizi hayo yalifanywa huwa linakumbwa pia mara kwa mara na mizozo ya mipaka baina ya Kaunti za Wajir na Garissa.
Ulinzi umeimarishwa na uchunguzi umeanzishwa kuhusu mashambulizi hayo ya jana (Novemba 22).