1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

Wanamgambo wa Somalia wawaua watu sita

6 Januari 2023

Wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali ya Somalia wamesema wapiganaji wa al-Shabaab leo wamewauwa watu wapatao sita wakati walipovamia kijiji cha katikati ya Somalia, ambapo walifukuzwa wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/4LpPC
Somalia Militants Twitter
Picha: picture alliance / AP Photo

Serikali ya Somalia na wapiganaji wa koo ambao ni washirika waliwafukuza wanamgambo hao kutoka kwenye maeneo waliyokuwa wanadhibiti tangu walipoanzisha operesheni kubwa mwezi Agosti.

Lakini al-Shabaab imelipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi kadhaa, ikiwemo kushambulia katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Siku ya Jumatano, al-Shabaab waliwaua takribani watu 35 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 40, baada ya mabomu mawili ya kutegwa kwenye gari kuripuka katika mji wa Mahas.

Hussein Aden, msemaji wa kundi la wapiganaji wa koo amesema shambulizi la leo limekilenga kijiji cha Hilowle Gaab kwenye jimbo la Hirshabelle.

Al-Shabaab imesema wamekiteka tena kijiji hicho na kukamata magari ya kijeshi na silaha, madai yanayopingwa na wakaazi na wanasiasa.