Wanajihadi wapoteza udhibiti wa Benghazi
26 Januari 2017Vikosi vya Libya vimeikamata wilaya kuu ya Benghazi kutoka kwa wapiganaji. Akithibitisha hayo, afisa mmoja mkuu wa jeshi amesema hiyo ni hatua kubwa katika vita vya kulidhibiti jiji hilo la mashariki.
Jamal al-Zahawi ambaye ni afisa wa kikosi maalum cha jeshi la Libya (LNA) ameliambia shirika la habari la Libya kuwa eneo la Ganfouda, tayari limekombolewa kikamilifu kutoka mikononi mwa magaidi.
Jamal ameongeza kuwa wapiganaji hao wanaoshukiwa kuwa na ufungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda wamelazimika kutorokea wilaya za karibu magharibi ya Benghazi. "Vita vyetu vya mwisho magharibi ya Benghazi vitakuwa katika katika majengo 12 ambamo magaidi wanajificha ndani.” Amesema Al-Zahawi huku akiongeza kuwa kikosi cha LNA kimefaulu kuwakomboa wafungwa 60 wa vita. Hakuna takwimu iliyotolewa kuhusu vifo.
Wanajeshi wa LNA ni waaminfu kwa utawala uliopo jiji la mashariki la Tobruk. Kudhibiti Ganfouda ni kati ya kampeni ya kijeshi iliyozinduliwa katikati ya mwaka 2014 chini ya mamlaka ya kiongozi jenerali Khalifa Haftar ambaye alisema lengo lake ni kuondoa waislamu wenye misimamo mikali nje kutoka Benghazi.
Mji wa Benghazi
Mji wa Benghazi ambao ni la pili kiukubwa nchini Libya, ni kati ya maeneo ya chimbuko la mapinduzi yaliyomaliza utawala wa miaka mingi ya Moamer Gaddafi. Tangu mapinduzi hayo, nchi hiyo ya Afrika kaskazini imekumbwa na mizozo ya kisiasa na ghasia za kiusalama.
Mwezi Machi mwaka 2016, serikali ya muungano inayoongozwa na Fayez Serraj na ambao pia unaungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ilichukua udhibiti wa mji mkuu Tripoli, huku kukiwa na matumaini ya kimataifa kuwa ingelimaliza ghasia katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.
Serikali hiyo ya Serraj, haijatambuliwa na wabunge walioko Tobruk, ambako pia ndiko serikali pinzani inakotokea.
Hata hivyo makundi ya jihadi yangali yanadhibiti wilaya za katikati za Benghazi za Al-Saberi na Souq al-Hout. Hayo ni kulingana na LNA. MAkundi hayo ya jihadi ni pamoja na Baraza la mapinduzi la Shura ambalo linashirikiana na wapiganaji wa kiislamu wanaojumuisha mtandao wa Al-Qaeda na Al-Sharia
Mwandishi: John Juma/ DPAE/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman