1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wanne wa Ujerumani wauliwa Baghlan karibu na Kundus nchini Afghanistan

Oumilkher Hamidou16 Aprili 2010

Wataliban wawauwa kwa mara nyengine tena wanajeshi wa Ujerumani wanaotumikia vikosi vya kimataifa kulinda amani nchini Afghanistan

https://p.dw.com/p/MyAz
Wanajeshi wa Ujerumani wanabeba jeneza la mwenzao kati ya wanne waliouliwaPicha: AP

Wanajeshi wanne wa Ujerumani wameuwawa kaskazini mwa Afghanistan. Hilo ni shambulio la pili la waasi wa Taliban katika kipindi cha siku chache tuu dhidi ya jeshi la shirikisho, Bundeswehr. Wanajeshi hao walikuwa wakipiga doria karibu na mji wa Baghlan, umbali wa kilomita 100 kusini mwa Kundus.

Wanajeshi walikua wakipiga doria kati ya kiunga kilichopo karibu na kambi yao huko Kundus na mji wa Baghlan ulioko umbali wa kilomita 100 hivi kutoka Kundus ,kisa hicho cha kikatili kilipotokea. Wanajeshi wa Ujerumani waliokuwa wakipiga doria walianza kufyetuliwa risasi,wanne kati yao wakauliwa na watano, kujeruhiwa. Kwa mujibu wa duru za jeshi la shirikisho, Bundeswehr, waasi waliwahujumu wanajeshi kwa makombora. Msemaji wa Taliban aliyezungumza kwa simu kutoka mahala pasipojulikana, amethibitisha kwamba wapiganaji wa Taliban wamekihujumu kifaru cha jeshi la Ujerumani kwa kombora. Hata hivyo kuna waliokuwa wakiitilia shaka ripoti hiyo. Polisi ya Afghanistan inazungumzia juu ya baruti. Opereshini ya kijeshi inayoendeshwa kwa pamoja kati ya wanajeshi wa Afghanistan na vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na jumuia ya kujihami ya NATO-ISAF, inaendelea.

Afghanistan Deutschland Bundeswehr Guttenberg in Feldlager Faisabad
Waziri wa ulinzi Karl-Theodor zu Guttenberg (kulia) akizungumza na wanajeshi katika kambi ya FaisabadPicha: AP

Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg, alipata habari za kuuwawa wanajeshi hao wanne wa Ujerumani alipokuwa njiani kurejea nyumbani baada ya ziara yake nchini Afghanistan. Akituwa kwa muda katika kituo cha jeshi la Ujerumani Bundeswehr cha Termes nchini Uzbekistan, waziri zu Guttenberg amethibitisha ripoti za kuuliwa wanajeshi hao wanne na kusema:

"Yaonyesha ulikuwa mtengo wa kikatili kabisa waliowekewa, lakini uchunguzi wa kina unahitajika na mie nitarejea haraka Afghanistan ili kuwa pamoja na wanajeshi wetu, ili kuweza kupata picha halisi ya yaliyotokea na zaidi kuliko yote kuwa pamoja na wanajeshi wetu."

Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani aliitembelea kambi ya kijeshi ya Kundus Jumatano iliyopita ili kujipatia picha halisi ya hali ya mambo baada ya kuuliwa wanajeshi watatu wa Ujerumani na wataliban siku ya Ijumaa kuu mwaka huu. Kutokana na kuzidi kuwa mbaya hali ya mambo katika maeneo ya kaskazini ya Afghanistan, waziri Karl-Theodor zu Guttenberg ameahidi silaha nzito nzito zitapelekwa nchini Afghanistan. Kwa namna hiyo wanajeshi wa Ujerumani wangepatiwa vifaru vyenye kinga dhidi ya hujuma za adui pamoja na vifaru vinavyobeba makombora ya kinga na makombora yenye uwezo wa kushambulia hadi umbali wa kilomita 40.

Mwandishi:Bosse, Ulrike/New Delhi NDR/ Hamidou Oumilkheir

Mpitiaji: Josephat Charo