1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi 4 wa Israel wauawa Jerusalem

9 Januari 2017

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema dereva wa lori hilo ni shabiki wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS

https://p.dw.com/p/2VUAP
Israel LKW-Anschlag in Jerusalem
Picha: Getty Images/AFP/A. Gharabli

Wanajeshi 4 wa Israel wameuawa na wengine 15 kujeruhiwa, baada ya mpalestina mmoja kuliendesha lori na kuwagonga mjini Jerusalem, punde waliposhuka kutoka kwenye basi. Watu 17 wamejeruhiwa kufuatia shambulio hilo. Msemaji wa polisi Luba Samri amesema, mshambuliaji aliyeliendesha lori hilo na kulielekeza kwa wanajeshi hao pia ameuawa kwa kupigwa risasi.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema dereva wa lori hilo ni shabiki wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS. Bila kutoa ushahidi, Netanyahu ameongeza kuwa shambulio hilo limechochewa kutokana na shambulio kama hilo barani Ulaya.

Katika siku za nyuma, Wapalestina wasiokuwa na uhusiano unaojulikana na kundi la IS wamekuwa wakifanya mashambulio kwa kutumia magari. Netanyahu amesema ''Tumemtambua mshambuliaji. Kulingana na dalili zote, alikuwa muungaji mkono wa IS. Tunajua kuwa kuna misururu ya mashambulio ya kigaidi. Bila shaka kutakuwa na uhusiano kati ya mashambulio hayo kwanzia Ufaransa, Berlin na sasa Jerusalem.''

Vikosi vya usalama vya Israel katika eneo la mkasa
Vikosi vya usalama vya Israel katika eneo la mkasaPicha: Getty Images/AFP/G. Tibbon

Picha za kamera za kiusalama za CCTV ambazo zimeneshwa katika vituo vya runinga nchini Israel zinaonesha lori likianja njia na kuendeshwa kwa mwendo wa kasi kuelekea kwenye umati wa watu uliokuwa Armon Hanatziv.

Shambulio hilo linajiri wakati wa wimbi la zaidi ya mwaka mmoja la mashambulizi ya risasi na visu yanayofanywa na Wapalestina dhidi ya Waisrael, ambayo yamepungua katika siku za karibuni.

Kisa hicho cha leo ndicho cha karibuni zaidi katika kipindi cha miezi mitatu cha maafa ya mashambulizi kwa Waisrael. Tangu Septemba mwaka 2015, Wapalestina wamewaua waisraeli 40.

Lakini katika kipindi hichohicho, Wapalestina 229 wameuawa na Waisraeli. Israel imesema ghasia hizo huchochewa na kampeni ya Palestine, huku Palestine ikisema ni matokeo ya takriban miaka 50 ya ukaliaji wa Israel  na matumaini yanayofifia kuhusu kuundwa kwa taifa huru la Wapalestina.