1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroNiger

Wanajeshi 10 wa Niger wauawa katika shambulio la wanamgambo

29 Septemba 2023

Wanajeshi 10 wa Niger wameuawa katika shambulio lililofanywa na wanamgambo kusini magharibi mwa nchi hiyo mapema jana asubuhi.

https://p.dw.com/p/4WwG9
Mwanajeshi wa Niger
Mwanajeshi wa NigerPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Vyanzo vitatu vya usalama vimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, shambulio hilo limefanyika takriban kilomita 190 kutoka mji mkuu Niamey karibu na mpaka wa Mali, Burkina na Niger.

Eneo hilo la Kandadji limekuwa kitovu cha oparesheni za waasi katika ukanda wa Sahel katika muda wa miaka michache iliyopita.

Vyanzo hivyo vikiwemo afisa mkuu wa kijeshi, viliomba kutotajwa majina yao kwa sababu hawajaidhinisha kuzungumza na vyombo na habari, japo hawakueleza ni kundi gani lililohusika na shambulio hilo.

Makundi ya wapiganaji wenye mafungamano na al-Qaeda na kundi linalojiita Dola la Kiislamu yamekuwa yakifanya mashambulizi ya mara kwa mara na kuwalenga wanajeshi na raia wa kawaida.