Wanadiplomasia wa G7 washikamana na Ukraine
4 Novemba 2022Mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la nchi saba zilizopiga hatua kiviwanda za G7 ambao wanakamilisha mkutano wa siku mbili katika mji wa kihistoria wa magharibi mwa Ujerumani wa Münster, wametoa taarifa ya kusisitiza msimamo wa pamoja kuhusu Ukraine, Urusi, China na yaliyojitokeza hivi karibuni nchini Iran na Korea Kaskazini.
Katika taarifa ya pamoja iliyowekwa katika tovuti ya wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani,mawaziri hao wa G7 kwa mara nyingine wametoa wito kwa Urusi kukomesha mara moja vita vyake dhidi ya Ukraine na kuondoa majeshi yake yote. Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, kwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba wanalaani ongezeko la hivi karibuni la mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya raia hasa ya maji na nishati kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani za Iran.
Wamesema kupitia mashambulizi hayo, Urusi inajaribu kuwatisha raia na kwamba mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia na miundombinu inaweza kuhesabiwa kuwa uhalifu wa kivita na kusisitiza azma ya kuhakikisha uwajibikaji kamili wa uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Mwaka mmoja baada ya kuonya juu ya athari za Urusi kuivamia Ukraine, mawaziri hao wa G7 wanatarajiwa kuidhinisha hatua zaidi za kuiadhibu Moscow na kuiunga mkono Kiev pamoja na mataifa yaliyoathirika kutokana na uhaba wa chakula na nishati kutokana na vita vinavyoendelea.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza James Cleverly amesema lengo la kundi hilo ni kufanya kila linalowezekana ili kuwasaidia Waukraine waweze kujilinda pamoja na kuwaunga mkono watu wengine ulimwenguni ambao wameathirika kutokana na uhaba wa chakula.
"Hilo ndilo tulikuwa tukijadili hapa na washirika wetu wa kimataifa katika G7 na marafiki zetu wanaotoka Afrika kuwakilisha sauti za wale ambao wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kwa sababu ya uchokozi wa Urusi dhidi ya Ukraine."
Kundi hilo limeitaka Urusi kurejea katika mkataba unaoruhusu usafirishaji salama wa nafaka kutoka Ukraine, kulingana na afisa mmoja mwandamizi wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.Viongozi wa G7 waazimia kukabiliana na kitisho cha njaa duniani
Kuhusu Iran, kundi hilo la G7 limelaani ukandamizaji wa Tehran dhidi ya wimbi la maandamano yaliyochcohewa na kifo cha msichana Mahsa Amini.
Aidha, wanadiplomasia hao wamelaani ongezeko la hivi karibuni la mvutano barani Asia unaosababishwa na ufyatuaji wa makombora ya Korea Kaskazini na kutoa onyo kali dhidi ya uwezekano wowote wa jaribio jipya la nyuklia.