1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walinda amani 3 wa Burundi wauawa Jamhuri ya Afrika ya Kati

26 Desemba 2020

Walinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa wameuawa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, huku nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi wa Jumapili (27 Disemba) na mapigano yakipamba moto kati ya vikosi vya serikali na waasi.

https://p.dw.com/p/3nE8X
Zentralafrikanische Republik | MINUSCA-Truppen auf Patrouille
Picha: ALEXIS HUGUET/AFP

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa inasema kuwa wanajeshi hao wanatokea Burundi na kwamba wenzao wawili wamejeruhiwa kufuatia uvamizi dhidi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa na vya serikali. 

Uvamizi huo ulifanyika kwenye mji wa Dekoa ulio katika mkoa wa Kemo na mji wa Bakouma kusini mwa mkoa wa Mbomou, ilisema taarifa hiyo bila kutaja undani zaidi.

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alilaani vikali mashambulizi hayo na kuzitaka mamlaka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kuchunguza kile alichokiita "uvamizi wa kikatili."

Pia alionya kwamba "mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuchukuliwa ni uhalifu wa kivita."

Taarifa hizo zimekuja katika wakati ambapo muungano wa waasi umetangaza kusitisha mapigano na kusema utaendelea na maandamano yake kwenye mji mkuu, Bangui, kufuatia kuwasili kwa vikosi vya Rwanda na Urusi kuilinda serikali ya taifa hilo lenye utajiri wa madini.

Bozize atuhumiwa

Zentalafrikanische Republik UN Mission MINUSCA
Vikosi vya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kati.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Kuelekea uchaguzi huo wa Jumapili (Disemba 27), Rais Faustin Archange Touadera anayewania tena wadhifa huo amemtuhumu mtangulizi wake, Francois Bozize, kwa kupanga njama ya mapinduzi. Lakini Bozize, ambaye amewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa na pia alizuwia na Mahakama ya Katiba kuwania urais, anakanusha shutuma hizo.

Siku ya Jumanne, kundi moja la wanamgambo liliuteka kwa muda mji wa nne kwa ukubwa nchini humo kabla ya mji huo kuchukuliwa tena na walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Makundi ya waasi yalianzisha mashambulizi wiki moja iliyopita yakitishia kuandamana kuelekea mji mkuu katika kile ambacho serikali inasema ni jaribio la mapinduzi.

Hata hivyo, kampeni hiyo ilisitishwa na msaada wa majeshi ya kimataifa.