Walibya waendelea kusubiri matokeo ya uchaguzi
9 Julai 2012Uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita nchini Libya ni wa kwanza huru kufanyika nchini humo katika muda wa miongo kadhaa. Mwasisi na mtu aliyepanga njama za uasi ambao uliuangusha utawala wa Moammar Gaddafi, ametoa wito wa kuwa na mazungumzo ya umoja wa kitaifa. Mahmud Jibril anayeongoza chama cha National Forces Alliances, ambacho kinasemekana kuwa kinaongoza kwa mujibu wa matokeo ya awali na yasiyo rasmi, ametoa wito kwa vyama vyote kuwa na umoja. Kiongozi huyo ametaka kufanyika majadiliano ya kitaifa, ili kufikiwa kwa muafaka, ambapo muswada wa katiba unaweza kuandikwa na serikali mpya inaweza kuundwa.
Matamshi yake yamekuja muda mfupi baada ya kiongozi wa chama cha Justice and Construction kukiri kuwa chama cha NFA kinaongoza katika uchaguzi huo katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, pamoja na mji wa pili kwa ukubwa wa Benghazi. Chama hicho kimepata matokeo mazuri katika miji mikubwa isipokuwa Misrata.
Akizungumza katika mkutano na wandishi wa habari uliofanyika hapo jana usiku, Jibril alisema "Hakuna mshindi wala aliyeshindwa katika uchaguzi uliofanyika. Kwa yeyote atakayeshinda, Libya ndiyo itakuwa imeshinda."
Waangalizi wa kimataifa waridhishwa na uchaguzi
Akiuzungumzia uchaguzi wa Jumamosi, mkuu wa kundi la waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya, Alexander Graf Lambsdorff, ameusifu kuwa hatua nzuri: "Uchaguzi huu ni mwanzo wa mchakato wa kidemokrasia. Ni lazima tuseme kwamba umekwenda vizuri kuliko tulivyotarajia. Uchaguzi huu umeweka msingi wa maendeleo ya kidemokrasia katika nchi hii. Lakini bado ipo kazi kubwa ya kufanya kwani nchi hii bado haina katiba." Lambsdorffaliongezea kuwa bado yapo maswali muhimu yanayohitaji majibu kama vile suala la kugawana mamlaka au kugawana mapato yatokanayo na uuzaji wa mafuta.
Uchaguzi wa Libya kwa sehemu kubwa ulikuwa shwari. Palikuwa na taarifa za hujuma katika baadhi ya vituo vya kupigia kura vilivyopo mashariki mwa nchi hiyo. Mtu mmoja aliuwawa katika mji wa Ajdabiya baada ya watu waliokuwa wamebeba silaha kukishambulia kituo kimoja cha kupigia kura kwa risasi. Lakini mbali na matukio hayo, zoezi la kupiga kura lilikwenda vizuri na watu wengi waliiona siku ya kupiga kura kama sikukuu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, kupitia msemaji wake amewapongeza Walibya kwa kupiga kura na kueleza kwamba zoezi zima lilikuwa limeandaliwa vizuri na kuendeshwa kwa uwazi. Ban amewataka Walibya sasa wakae pamoja na kutunga katiba mpya ya haki na itakayoleta maridhiano huku ikiyajumuisha makundi yote katuka jamii
Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef