Wakurdi, Serikali ya Syria kushirikiana dhidi ya Uturuki
14 Oktoba 2019Katika tangazo lake kwa vyombo vya habari, utawala wa Wakurdi umesema makubaliano ya ushirikiano na serikali ya Syria yamefikiwa kwa lengo la kuzuia walichokiita uchokozi. Tangazo hilo limeongeza kuwa wanajeshi wa serikali ya Syria watapelekwa kwenye mpaka biana ya Syria na Uturuki kupigana bega kwa bega na vikosi vya Kikurdi vijulikanavyo kama Syrian Democratic Forces, SDF.
Sambamba na kutolewa kwa tangazo hilo la Wakurdi, shirika la habari la Syria, SANA limeripoti kuwa tayari jeshi la serikali ya rais Bashar al-Assad lilikuwa likituma vikosi katika mji wa Tal Tamr kwenye mpaka na Uturuki.
Chaguo kati ya kusalimu amri na kuangamia
Wapiganaji wa Kikurdi wamekuwa wakilemewa na operesheni za jeshi la Uturuki lenye nguvu zaidi, na kamanda mkuu wa SDF Mazlum Abdi amesema katika makala yake kwenye jarida la Sera ya Kigeni, kuwa wanakabiliwa na chaguo gumu kati ya kuridhia matakwa ya serikali ya Syria, na maangamizi dhidi ya watu wao, akisema bila shaka maisha ya watu ndiyo yenye kipaumbele.
Wakurdi wamejikuta katika hali ngumu baada ya mshirika wao wa muda mrefu, Marekani kuamua kuondoa wanajeshi wao katika eneo wanalolithibiti kaskazini mwa Syria, na kuacha pengo lililotumiwa na Uturuki kuingia kijeshi kuwawinda Wakurdi hao ambao inawaita magaidi.
Awali Marekani iliwaondoa wanajeshi wachache tu, lakini sasa waziri wake wa ulinzi Mark Esper amezungumzia uwezekano wa kuwahamisha pia wanajeshi wote waliosalia katika eneo hilo.
''Tumejikuta katika mazingira ambapo wanajeshi wa Kimarekani wamenaswa katikati ya majeshi mawili hasimu, hali ambayo haidhibitiki. Kwa hiyo nimezungumza na rais, baada ya kushauriana na maafisa wengine wa usalama wa taifa'' amesema waziri Esper, na kuongeza kuwa rais Trump ''ametoa amri ya kuanza zoezi la kuviondoa vikosi vyetu kutoka kaskazini mwa Syria.''
Maisha ya raia yazidi kupotea
Operesheni hii ya kijeshi iliyoanzishwa na Uturuki kaskazini mwa Syria Jumatano iliyopita tayari imeuwa raia zaidi ya 60 upande wa Syria, huku duru za Uturuki zikieleza kuwa upande wa nchi hiyo, raia 18 wamepoteza maisha kutokana na makombora yanayorushwa na Wakurdi.
Hapo jana, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alizungumza kwa njia ya simu na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, na kumhimiza kusimamisha mara moja operesheni hizo, kwa hoja kwamba zinawalazimisha maelfu ya watu kuyakimbia makaazi yao, kuyumbisha usalama wa kikanda na kulipa nguvu mpya kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.Ufaransa imeutaka Umoja wa Ulaya kulaani operesheni hizo za kijeshi za Uturuki, namuiwekea vikwazo vya silaha nchi hiyo.
afpe,ape