Wakimbizi wa Somalia wajuta kurejeshwa nyumbani
27 Juni 2017Watoto wengi wanajuta kurejea nchini Somalia kutoka Kenya walipoishi kama wakimbizi.
Aden Hussein, ni kijana aliyeamua kuishi kama mkimbizi ili kupata elimu. Wakati Somalia ikiendelea kukabiliwa na machafuko aliamua kukimbilia Kenya akiiacha familia yake na kuishi katika kambi ya wakimbizi iliyo kubwa zaidi na ya muda mrefu duniani ya Dadaab nchini Kenya, iliyo chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za misaada.
"Kule ninapata elimu ya bure", ameliambia shirika la habari la AFP.
Agosti mwaka jana, ikiwa ni miaka sita baada ya kufika kwenye kambi hiyo, Hussein mwenye miaka 21 alipata kitita cha fedha za kurejeshwa makwao zilizotolewa kwa wakimbizi wa Somalia baada ya serikali ya Kenya kutangaza mpango wake kuifunga kambi hiyo.
Hussein alisema alipatiwa kiasi cha Dola 400 na kuahidiwa kupata huduma za kiafya, makazi na elimu, mafao ambayo alifaidika nayo alipokuwa akiishi Dadaab.
Mashirika yanayoangazia haki za binaadamu yalipinga hatua hiyo kwa kusema wakimbizi hao walikuwa wakikosewa haki kwa kurejeshwa katika eneo linalokabiliwa na vita na hakuna huduma za kiutu zinazopatikana huko. Lakini mwisho wa yote, Hussein alipatiwa kiasi hicho cha fedha.
Alifadhaishwa sana kwa kuwa hakufanikiwa kumaliza elimu yake ya sekondari tangu aliporejea katika mji wa Baidoa, uliopo Kusinimagharibi mwa Somalia.
Katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, zaidi ya wakimbizi 50,000 waliondoka Dadaab na kurudi Somalia, taifa linalochukuliwa kama lililovurugika tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 1991.
Miongoni mwa majeruhi yalitokana na machafuko hayo ni mfumo wa kitaifa wa elimu ambao serikali dhaifu za mfululizo nchini humo zimeshindwa kuujenga upya.
Baadhi ya shule zilizoko nje ya miji mikubwa ni za masomo ya Kiislamu, madrasa na nyingine ambazo zinaendelea kutoa elimu, zikiwa na walimu wasio na taaluma ya kutosha ya ualimu ama mitaala yenye viwango visivyokubalika.
Mtafiti wa Somalia, katika shirika la haki ya binaadamu la Amnesty International, Patrick Mbugua ambaye amerejea hivi karibuni kutoka katika mji wa Baidoa alikokuwa akifanya tafiti, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wengi wa wakimbizi aliozungumza nao walisema watoto wao hawaendelei tena na masomo. Na wale waliorejea shuleni walikuta mifumo ya elimu ikiwa imevurugika.
Kati ya shule 29 katika mji wa Baidoa, baadhi zinaendeshwa na watu binafsi na zinafuata mitaala ya Ethiopia, Kenya, Uganda ama hata Qatar, huku shule za umma zikisalia katika mitaala ile ile ya Somalia, iliyopitwa na wakati na iliyokuwepo kabla ya kuanza kwa zama za vita na haijabadilika kwa zaidi ya miaka 20.
Kinyume na hilo, shule zote katika kambi ya Dadaab zinafuata mtaala ya kisasa zaidi wa Kenya.
Mfumo wa elimu wa Somalia, haufanyi kazi kikamilifu, na bado unakabiliwa na changamoto, afisa wa mahusiano ya nje wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Julien Navier ameiambia AFP. Navier amesema wazazi waliorejeshwa Somalia wanaweza kuchagua kuwabakiza watoto wao kwenye shule zinazofuata mfumo wa Kenya.
Kukosekana kwa ushirikiano kati ya serikali kuu ya Somalia na majimbo ya taifa hilo pia kunasababisha changamoto. Afisa mwandamizi wa elimu katika mji wa Baidoa, Sadad Mohamed Nur amesema idara yake iko tayari kusaidia suala la elimu, lakini ameilaumu serikali kuu kwa kushindwa kutoa fedha.
Mwandishi: Lilian Mtono/afp
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman