1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu waanza mfungo wa mwezi wa Ramadhani

24 Aprili 2020

Waislamu kote ulimwenguni wanaanza ibada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, katikati ya sintofahamu inayotokana na hatua za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona ambazo ni Pamoja na kuwazuia watu kutoka nje.

https://p.dw.com/p/3bM5M
Coronavirus | Bangladesch | Moschee
Picha: DW/H. Ur Rashid Swapan

Waislam waanza mfungo wa mwezi wa Ramadhan

Virusi vya corona kwa kiasi kikubwa vimebadilisha mfumo wa Maisha duniani, huku mataifa yakipambana kwa kila hali kukabiliana na maradhi yanayosababishwa na virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19. Karibu vifo 190,000 vimetokea kutokana na ugonjwa huo, idadi ya walioambukizwa hivi sasa inakaribia milioni 2.7, na pia uchumi wa dunia umeathirika pakubwa.

Waumini wa dini ya Kiislamu kuanzia Kusini Mashariki mwa Asia hadi Mashariki ya Kati na hata Afrika wanaanza mwezi huu mtukufu katikati kadhia ya mapambano haya, kwa kuzuiwa kukusanyika na hata kutoka nje.

Hawaruhusiwi kukusanyika kwa ibada misikitini na hata kufanya mikusanyiko mikubwa ya kifamilia pamoja na marafiki wakati wa futari nyakati za jioni baada ya siku nzima ya mfungo, kama ilivyozoeleka.

Hata hivyo licha ya kitisho kinacholetwa na virusi vya corona, viongozi wa dini na wahafidhina katika mataifa mengi kama Bangladesh, Pakistan na Indonesia ambayo yanakaliwa na idadi kubwa ya Waislamu, wanapuuzilia mbali sheria za kutokukusanyika na kuendelea kwenda misikitini.

Maelfu ya watu walihudhuria ibada ya jioni jana Alhamisi iliyofanyika kwenye msikiti mkubwa uliopo kwenye mji mkuu wa Indonesia na kulishuhudiwa mikusanyiko kama hiyo katika maeneo mengi nchini Pakistan.

WHO yaomba shughuli za kawaida zinazofanyika wakati wa ramadhani kusimamishwa

WHO in Genf | Coronavirus | Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Getty Images/AFP

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limetoa mwito wa kusimamishwa kwa baadhi ya shughuli ambazo hufanyika katika mwezi wa Ramadhan ili kupunguza kitisho cha kusambaa zaidi kwa virusi vya corona, huku mamlaka katika mataifa mbalimbali zikionya kuhusu kitisho kilichopo iwapo watu watakusanyika.

Kumetokea mripuko wa maambukizi ya virusi vya corona katika mikusanyiko mitatu tofauti ya waumini wa Kiislamu nchini Malaysia, Pakistan na India tangu kulipotangazwa kuibuka kwa virusi hivyo mwaka jana nchini China.

Hatua za kujizuia na mikusanyiko pamoja na athari mbaya kabisa za kiuchumi kufuatia janga hilo pia kunamaanisha kwamba hata mashirika mengi ambayo hutoa misaada wakati wa mwezi huu, na hususan kugawa vyakula na misaada mingine, pia yameathirika vibaya.

Raia mmoja wa Palestina, Salah Jibril anayeishi na familia yake yenye watoto sita katika chumba kimoja kibovu katika eneo la ukanda wa Gaza amesema hata hajui namna familia yake itakavyoishi bila ya misaada kutoka kwenye mashirika kama hayo.

Masoko na misikiti vyote vimefungwa, watu wazuri wanaotupatia fedha ama misaada kila Ramadhan nao wanakabiliwa na hali ngumu, alilalama Jibril. Akasema, hii ni Ramadhani ngumu mno ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Chanzo:AFP