1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wataka hatua dhidi ya ukosefu wa ajira

Abdu Said Mtullya22 Mei 2012

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya ripoti ya Shirika la Kazi Duniani, ILO kuhusu ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kusini mwa Ulaya.

https://p.dw.com/p/14ztL
Vijana wasiokuwa na ajira nchini Uhispania
Vijana wasiokuwa na ajira nchini UhispaniaPicha: AP

Juu ya ripoti ya Shirika la Kazi Duniani,ILO kuhusu ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana barani Ulaya gazeti la "Südwest -Presse" linasema takwimu za shirika hilo juu ya ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana zinatisha.Lakini linasema jambo baya zaidi ni kutambua kwamba hali hiyo itakuwa ya muda mrefu. Mhariri wa "Südwest-Presse" anasema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana ni hatua ya kusikitisha sana katika historia ya hivi karibuni barani Ulaya.

Mhariri huyo anasikitika kwa kusema kuwa vijana wengi wenye elimu nzuri,nchini Uhispania ambao hivi karibuni walitumai kuwa na maisha mazuri kuliko ya wazazi wao sasa wanapaswa kufanya kazi za kubabaisha ili kuendesha maisha yao. Rika zima la vijana limo katika hatari ya kutelezea katika umasikini.


Gazeti la"Donaukurier"pia linazungumzia juu ya ripoti ya shirika la kazi duniani kuhusu ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani umuhimu wa kuwa na mipango ya muda mrefu ya kulitatua tatizo hilo.

Anasema kuwaajiri nchini Ujerumani, vijana kutoka kusini mwa Ulaya kutakuwa suluhisho la muda mfupi tu.Tatizo ni kwamba vijana wenye ujuzi wataondoka katika nchi zao zenye matatizo. Na kwa hivyo patakuwa na ukosefu wa vijana wa kuujenga uchumi wa nchi zao. Kilichobakia sasa,kwa nchi za Ulaya na hasa zilizomo katika Umoja wa sarafu ya Euro ni kuangalia pia nje ya mawanda ya kubana matumizi ili kuweza kuleta ustawi wa uchumi.

Viongozi wa nchi za mfungamano wa kijeshi wa NATO wameafikiana juu ya kuyaondoa majeshi ya mfungamano wao kutoka Afghanistan mnamo mwaka wa 2014. Jee nini kitatokea baada ya hapo? Mhariri wa gazeti la "Heilbronner Stimme"anatoa maoni yake kwa kusema kuwa baada ya Afghanistan,NATO itakabiliwa na changamoto nyingine, yaani mpango wa barani Ulaya wa kujihami dhidi ya makombora,mkakati wa ulinzi dhidi ya Iran.

Kwa mara nyingine mpango huo unatokana na sera za Marekani, utakaotekelezwa na NATO. Mhariri anasema iwapo ulinzi huo wa gharama kubwa una manufaa yoyote, na iwapo pana haja yoyote ya kuzozana na Urusi,ni jambo la mjadala.

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" katika maoni yake linamtetea Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaelaumiwa kwa kuiteketeza sarafu ya Euro kutokana na msimamo wake thabiti juu kubana matumizi.Mhariri wa gazeti hilo anasema mtazamo huo ni kuukanganya ukweli. Anasema hali halisi ni kwamba, matatizo ya eneo la nchi za Umoja wa sarafu ya Euro ni sawa na yale ya nchini, Japan na Marekani. Hayatokani na sera za kubana matumizi bali yanatokana na madeni yasiyokuwa na kikomo. Mabilioni yaliyotokana na mikopo yaliyoekezwa kwa ajili ya kutenga nafasi za ajira yamechochea moto wa nyasi kavu tu !

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Abdul-Rahman