Wageni na Dini kujumuishwa katika kampeni ya uchaguzi Ufaransa
7 Machi 2012Rais Nicolas Sarkozy anataka kuzidisha makali ya sera za uhamiaji pindi akichaguliwa tena,akilenga kupunguza kwa nusu idadi ya wageni wanaoingia kila mwaka nchini humo pamoja pia na kupunguza huduma za jamii kwa wahamiaji.
"Mfumo wetu wa kuwakaribisha wageni haufanyi kazi vizuri kwasababu kuna wageni wengi kupita kiasi katika nchi yetu,na hatuwezi tena kuwapatia makaazi,ajira wala shule" amesema rais Sarkozy jana usiku katika mahojiano pamoja na kituo cha televisheni cha Ufaransa France Deux .
"Katika mhula ujao wa miaka mitano,nnahisi ili kuanzisha mipango ya maana ya kuwakaribisha vyema wageni itabidi idadi ya watu tunaowakaribisha ipunguzwe mara dufu,kutoka watu laki moja na 80 elfu na kusalia watu laki moja."Amesisitiza rais Nicolas Sarkozy.
Akitajikana kupitwa vibaya sana na mgombea wa chama cha kisoshialisti cha Ufaransa Francois Hollande, uchaguzi wa rais utakapoitishwa kwanza April 22 na baadae May 6,rais Sarkozy anaonekana kuzipigia upatu mada zile zile za uhamiji na usalama zilizompatia ushindi katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2007.
Kwa mara ya kwanza rais Sarkozy amezungumzia mipango ya kuwekewa vizuwizi wageni katika kupokea huduma za jamii ambazo hadi wakati huu zilikuwa sawa kwa watu wote wanaoishi kuambatana na sheria nchini Ufaransa.
Katika wakati ambapo chama tawala cha kihafidhina cha UMP kinawatuhumu wafuasi wa mrengo wa shoto kuwa ndio chanzo cha kumiminika mikururo ya wahamiaji,hata hivyo takwimu rasmi zilizolifikia shirika la habari la Ufaransa AFP zinaonyesha rikodi ya wahamiaji imevunjwa katika utawala wa wahafidhina walipoingia wahamiaji laki mbili na 40 elfu mnamo mwaka 2004.
Mrengo wa shoto unamlaumu Sarkozy na washirika wake wa karibu kwa kufuata sera za wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia kwa lengo la kujikusanyia kura zaidi kwaajili ya uchaguzi ujao wa rais.
Jumamosi iliyopita rais Sarkozy alisema haki ya wageni ambao hawatokei katika nchi za Umoja wa ulaya,kupiga kura katika chaguzi za mabaraza ya miji-kama wanavyopendekeza wapinzani wake wa chama cha kisoshialisti ni sawa na "kuichafua jamhuri".
Mvutano mkali umezuka pia kuhusiana na nyama inayochinjwa kuambatana na utaratibu wa dini ya kiislam na kiyahudi,baada ya waziri mkuu Francois Fillon kushuri waumini wa dini hizo waachane na kile alichokiita "desturi za kale" za kuchinja wanyama ambazo anahoji "hazina tena maana ".Matamshi hayo yamezusha lawama kutoka wakuu wa jamii za wayahudi na waislam nchini Ufaransa.Katika mahojiano yake kwa njia ya televisheni jana usiku,rais Nicolas Sarkozy amekanusha kwamba kambi yake inafuata nyayo za wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir//AFP
Mhariri:Josephat Charo