1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa upinzani Uganda warejea bungeni

29 Novemba 2023

Wabunge wa upinzani nchini Uganda wamerudi bungeni baada ya kususia vikao kwa zaidi ya mwezi mmoja.

https://p.dw.com/p/4Zarc
Siasa | Bunge la Uganda likiwa katika vikao vya kawaida
Bunge la Uganda likiwa katika mikutano yake ya kawaidaPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Hii ni baada ya spika wa bunge Anita Among kuwarai huku akimshinikiza waziri wa masuala ya ndani na yule wa usalama kuwasilisha taarifa kuhusu watu wanaodaiwa na upinzani kutoweka baada ya kukamatwa na vyombo vya dola.

Spika aliorodhesha suala la wabunge wa upinzani kwa mara ya kwanza kwenye ratiba ya shughuli za bunge na wabunge wa upinzani walipoiona wakakubali kurejea bungeni.

Lakini hii ilikuwa baada ya kutokea vurugu chache wakati baadhi ya wabunge wa chama tawala NRM na wengine wa upinzani walipotupiana maneno na kusababisha polisi wa bungeni kuingilia kati kuidhibiti hali.

Soma pia:Polisi Uganda yazuwia mapokezi ya Bobi Wine

Leo waziri wa masuala ya ndani Kahinda Otafire, amewasilisha taarifa bungeni kuitikia hoja zilizowafanya wabunge wa upinzani kuanza kususia vikao.

Wiki iliyopita, spika alitishia kutangaza viti vyawabunge wa upinzani kuwa wazi, jambo ambalo lingesababisha kufanyika uchaguzi mdogo.