1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Libya waridhia baraza jipya la mawaziri

Sylvia Mwehozi
10 Machi 2021

Bunge la Libya limepiga kura kuipitisha serikali ya Umoja wa kitaifa inayoongozwa na waziri mkuu AbdulHamid Dbeibah kama sehemu ya mpango wa kuutafutia ufumbuzi mzozo wa muda mrefu kueleka uchaguzi wa mwezi Desemba

https://p.dw.com/p/3qRWu
Libyen Parlament
Picha: Esam Omran Al-Fetori/REUTERS

Bunge hilo limeidhinisha baraza la mawaziri lililopendekezwa na waziri mkuu Dbeibeh kwa kura 132 za ndio dhidi ya 2 za hapana, katika kikao kisicho cha kawaida kwenye mji wa Sirte. Kuidhinishwa kwa serikali hiyo kunatoa fursa muhimu baada ya muda mrefu wa juhudi za utatuzi wa mgogoro wa Libya. Mara baada ya kura hiyo Waziri mkuu Dbeibeh alilieleza bunge kuwa kupitia kura hiyo ni dhahiri kwamba Walibya ni wamoja. 

Katika mitaa ya Libya, biashara na taasisi za serikali zimebaki katika kivuli cha makundi yaliyo na silaha na mgawanyiko baina ya tawala mbili zinazokinzana, wakati mataifa ya kigeni yanayounga mkono pande tofauti yakikaidi kuondoa silaha zake. Kuitishwa kwa uchaguzi huru wa bunge na rais katika mazingira kama hayo mwishoni mwa mwaka huu kutakuwa ni changamoto kubwa, ingawa pande zote zimeahidi kuheshimu.

Libyen I Abdul Hamid Dbeibah
Waziri mkuu mteule wa Libya Abdul Hamid DbeibahPicha: Mucahit Aydemir/AA/picture alliance

Kikao cha bunge kimefanyika katika mji wa Sirte, ambako makabiliano yalitulia wakati wa majira ya kiangazi baada ya serikali inayotambulika kimataifa ya Umoja wa kitaifa GNA, ilipolifurusha jeshi la kitaifa la Libya LNA kutoka Tripoli chini ya kamanda Khalifa Haftar lenye makao yake makuu mashariki mwa Libya.

Kikao hicho cha bunge ni cha kwanza na kamilifu ndani ya miaka mingi baada ya bunge hilo kugawanyika kati ya mashariki na magharibi muda mchache baada ya kuchaguliwa mwaka 2014.

Awali Waziri Mkuu Dbeibah aliwataka takribani wapiganaji wa kigeni 20,000 waondoke nchini humo akisema mamluki wanaohudumu nchini humo ni wasaliti na kwamba ataufahamisha Umoja wa Mataifa na nchi wanakotoka wapiganaji hao.

Dbeibah alilaani kile alichokiita kampeni kali inayofanywa na wale wanaotaka kuiharibu nchi hiyo, kwa lengo la kuikalia.

Mchakato huo wa Umoja wa Mataifa unalenga kuiunganisha nchi hiyo baada ya mpango wa kusitisha mapigano uliofikiwa Oktoba kati ya serikali mbili pinzani.

Dbeibah alichaguliwa mwezi uliopita katika mazungumzo yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa, na kuhudhuriwa na vikundi tofauti vya Libya ili kulipitisha taifa hilo kuelekea uchaguzi wa Desemba. Serikali hiyo ya mpito sasa itakuwa na kibarua kigumu cha kushughulikia matatizo chungunzima ya Walibya, kuanzia mdororo wa uchumi na ongezeko la ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei na kuzorota kwa huduma za umma.